마태복음 15장 Swahili NT
- 1 Kisha Mafarisayo na walimu wa Sheria wakafika kutoka Yerusalemu, wakamwendea Yesu, wakamwuliza,
- 2 "Kwa nini wanafunzi wako hawajali mapokeo tuliyopokea kutoka kwa wazee wetu? Hawanawi mikono yao kama ipasavyo kabla ya kula!"
- 3 Yesu akawajibu, "Kwa nini nanyi mnapendelea mapokeo yenu wenyewe na hamuijali Sheria ya Mungu?
- 4 Mungu amesema: Waheshimu baba yako na mama yako, na Anayemkashifu baba yake au mama yake, lazima auawe.
- 5 Lakini ninyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba au mama yake, lakini akasema: Kitu hiki nimemtolea Mungu,
- 6 basi, hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa kufuata mafundisho yenu wenyewe.
- 7 Enyi wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu:
- 8 Watu hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno tu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami.
- 9 Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu."
- 10 Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, "Sikilizeni na muelewe!
- 11 Kitu kinachomtia mtu najisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu najisi."
- 12 Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, "Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?"
- 13 Lakini yeye akawajibu, "Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakuupanda, utang'olewa.
- 14 Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni."
- 15 Petro akadakia, "Tufafanulie huo mfano."
- 16 Yesu akasema, "Hata nyinyi hamwelewi?
- 17 Je, hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutupwa nje chooni?
- 18 Lakini yale yatokayo kinywani hutoka moyoni, na hayo ndiyo yanayomtia mtu najisi.
- 19 Maana moyoni hutoka mawazo maovu yanayosababisha uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na kashfa.
- 20 Hayo ndiyo yanayomtia mtu najisi. Lakini kula chakula bila kunawa mikono hakumtii mtu najisi."
- 21 Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni.
- 22 Basi, mama mmoja Mkaanani wa nchi hiyo alimjia, akapaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo."
- 23 Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, "Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele."
- 24 Yesu akajibu, "Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo."
- 25 Hapo huyo mama akaja, akapiga magoti mbele yake, akasema, "Mheshimiwa, nisaidie."
- 26 Yesu akamjibu, "Si sawa kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa."
- 27 Huyo mama akajibu, "Ni kweli, Mheshimiwa; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao."
- 28 Hapo Yesu akamjibu, "Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka." Yule binti yake akapona tangu saa hiyo wakati huohuo.
- 29 Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi.
- 30 Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya.
- 31 Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; wakamsifu Mungu wa Israeli.
- 32 Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, "Nawaonea watu hawa huruma kwa sababu kwa siku tatu wamekuwa nami, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende bila kula wasije wakazimia njiani."
- 33 Wanafunzi wakamwambia, "Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?"
- 34 Yesu akawauliza, "Mnayo mikate mingapi?" Wakamjibu, "Saba na visamaki vichache."
- 35 Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini.
- 36 Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu.
- 37 Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya makombo, wakajaza vikapu saba.
- 38 Hao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto.
- 39 Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.