마태복음 4장 Swahili NT
- 1 Kisha Roho alimwongoza Yesu mpaka jangwani ili ajaribiwe na Ibilisi.
- 2 Akafunga siku arubaini mchana na usiku, na mwishowe akaona njaa.
- 3 Basi, mshawishi akamjia, akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate."
- 4 Yesu akamjibu, "Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: Binadamu hataishi kwa mikate tu, ila kwa kila neno asemalo Mungu."
- 5 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, mji mtakatifu, akamweka juu ya mnara wa hekalu,
- 6 akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini; maana imeandikwa: Mungu atawaamuru malaika wake kwa ajili yako; watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe."
- 7 Yesu akamwambia, "Imeandikwa pia: Usimjaribu Bwana, Mungu wako."
- 8 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka juu ya mlima mrefu, akamwonyesha falme zote za ulimwengu na fahari zake,
- 9 akamwambia, "Hivi vyote nitakupa kama tu ukipiga magoti na kuniabudu."
- 10 Hapo, Yesu akamwambia, "Nenda zako Shetani! Imeandikwa: Utamwabudu Bwana Mungu wako na kumtumikia yeye peke yake."
- 11 Basi, Ibilisi akamwacha, na malaika wakaja, wakamhudumia.
- 12 Yesu aliposikia kwamba Yohane ametiwa gerezani alikwenda Galilaya.
- 13 Aliondoka Nazareti, akaenda Kafarnaumu, mji ulio kando ya bahari ya Genesareti, mpakani mwa wilaya za Zabuloni na Naftali, akakaa huko.
- 14 Ndivyo lilivyotimia lile neno lililosemwa kwa njia ya nabii Isaya:
- 15 "Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, kuelekea baharini ng'ambo ya mto Yordani, Galilaya nchi ya watu wa Mataifa!
- 16 Watu waliokaa gizani wameona mwanga mkubwa. Nao walioishi katika nchi ya giza na kivuli cha kifo, mwanga umewaangazia!"
- 17 Tangu wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, "Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia!"
- 18 Yesu alipokuwa anatembea kando ya ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili wavuvi; Simoni (aitwae Petro) na Andrea, ndugu yake; walikuwa wakivua samaki kwa nyavu ziwani.
- 19 Basi, akawaambia, "Nifuateni, nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu."
- 20 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.
- 21 Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona ndugu wengine wawili: Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Hao walikuwa ndani ya mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakitengeneza nyavu zao. Basi Yesu akawaita,
- 22 nao mara wakaiacha mashua pamoja na baba yao, wakamfuata.
- 23 Yesu alikuwa anakwenda kila mahali wilayani Galilaya, akifundisha katika masunagogi na kuhubiri Habari Njema juu ya ufalme wa Mungu. Aliponya kila namna ya maradhi na magonjwa waliyokuwa nayo watu.
- 24 Habari zake zikaenea katika mkoa wote wa Siria. Wagonjwa wote wenye maradhi ya kila namna na wale waliosumbuliwa na kila namna ya taabu: waliopagawa na pepo, wenye kifafa na watu waliokuwa wamelemaa, walipelekwa kwake; naye akawaponya wote.
- 25 Makundi mengi ya watu kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea na ng'ambo ya mto Yordani, walimfuata.