마태복음 7장 Swahili NT
- 1 "Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu;
- 2 kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu.
- 3 Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako?
- 4 Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako, wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako?
- 5 Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako na hapo ndipo utaona waziwazi kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichoko jichoni mwa ndugu yako.
- 6 "Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua ninyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga.
- 7 "Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni, nanyi mtafunguliwa.
- 8 Maana, aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye hufunguliwa.
- 9 Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe?
- 10 Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka?
- 11 Kama basi ninyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: atawapa mema wale wanaomwomba.
- 12 "Watendeeni wengine yale mnayotaka wao wawatendee ninyi. Hii ndiyo maana ya Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii.
- 13 "Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi.
- 14 Lakini njia inayoongoza kwenye uzima ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.
- 15 "Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali.
- 16 Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La!
- 17 Basi, mti mwema huzaa matunda mema, na mti mbaya huzaa matunda mabaya.
- 18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mema.
- 19 Kila mti usiozaa matunda mema utakatwa na kutupwa motoni.
- 20 Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao.
- 21 "Si kila aniambiaye, Bwana, Bwana, ataingia katika Ufalme wa mbinguni; ila ni yule tu anayetimiza mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
- 22 Wengi wataniambia Siku ile ya hukumu: Bwana, Bwana! kwa jina lako tulitangaza ujumbe wako, na kwa jina lako tuliwatoa pepo na kufanya miujiza mingi.
- 23 Hapo nitawaambia: Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni mbele yangu, enyi watenda maovu.
- 24 "Kwa sababu hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba.
- 25 Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba.
- 26 "Lakini yeyote anayesikia maneno yangu haya bila kuyazingatia, anafanana na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga.
- 27 Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo ikaanguka; tena kwa kishindo kikubwa."
- 28 Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, umati wa watu ukashangazwa na mafundisho yake.
- 29 Hakuwa kama walimu wao wa Sheria, bali alifundisha kwa mamlaka.