마가복음 13장 Swahili NT
- 1 Yesu alipokuwa anatoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, "Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!"
- 2 Yesu akamwambia, "Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa."
- 3 Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea Hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha,
- 4 "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?"
- 5 Yesu akaanza kuwaambia, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.
- 6 Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, wakisema, Mimi ndiye! nao watawapotosha watu wengi.
- 7 Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado.
- 8 Taifa moja litapigana na taifa lingine; utawala mmoja utapigana na utawala mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto.
- 9 "Lakini ninyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu ili mpate kunishuhudia kwao.
- 10 Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote.
- 11 Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si ninyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu.
- 12 Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanae; watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua.
- 13 Watu wote watawachukieni ninyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.
- 14 "Mtakapoona Chukizo Haribifu limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake!) Hapo watu walioko Yudea wakimbilie milimani.
- 15 Mtu aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu.
- 16 Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.
- 17 Ole wao waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!
- 18 Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi.
- 19 Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena.
- 20 Kama Bwana asingepunguza siku hizo, hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo.
- 21 "Basi mtu akiwaambieni, Tazama, Kristo yupo hapa! au Yupo pale! msimsadiki.
- 22 Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, ili kuwapotosha wateule wa Mungu, kama ikiwezekana.
- 23 Lakini ninyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea.
- 24 "Basi, siku hizo baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza.
- 25 Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.
- 26 Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu.
- 27 Kisha atawatuma malaika wake; atawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.
- 28 "Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
- 29 Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana.
- 30 Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.
- 31 Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
- 32 "Lakini hakuna mtu ajuaye siku au saa hiyo itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye.
- 33 Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini.
- 34 Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia mlinzi wa mlango awe macho.
- 35 Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi.
- 36 Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala.
- 37 Ninayowaambieni ninyi, nawaambia wote: Kesheni!"