마가복음 7장 Swahili NT
- 1 Baadhi ya Mafarisayo na walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikusanyika mbele ya Yesu.
- 2 Waliona kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikula mikate kwa mikono najisi, yaani bila kunawa.
- 3 Maana Mafarisayo na Wayahudi wengine wote huzingatia mapokeo ya wazee wao: hawali kitu kabla ya kunawa mikono ipasavyo.
- 4 Tena hawali kitu chochote kutoka sokoni mpaka wamekiosha kwanza. Kuna pia desturi nyingine walizopokea kama vile namna ya kuosha vikombe, sufuria na vyombo vya shaba.
- 5 Basi, Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, "Mbona wanafunzi wako hawayajali mapokeo tuliyopokea kwa wazee wetu, bali hula chakula kwa mikono najisi?"
- 6 Yesu akawajibu, "Wanafiki ninyi! Nabii Isaya alitabiri ukweli juu yenu alipoandika: Watu hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno matupu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami.
- 7 Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.
- 8 Ninyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu."
- 9 Yesu akaendelea kusema, "Ninyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu.
- 10 Maana Mose aliamuru: Waheshimu baba yako na mama yako, na, Anayemlaani baba au mama, lazima afe.
- 11 Lakini ninyi mwafundisha, Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani ni zawadi kwa Mungu),
- 12 basi, halazimiki tena kuwasaidia wazazi wake.
- 13 Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo."
- 14 Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, "Nisikilizeni nyote, mkaelewe.
- 15 Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu toka nje ambacho chaweza kumtia mtu najisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu najisi."
- 16 Mwenye masikio na asikie!
- 17 Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano.
- 18 Naye akawaambia, "Je, hata ninyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu toka nje hakiwezi kumtia unajisi,
- 19 kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?" (Kwa kusema hivyo, Yesu alivihalalisha vyakula vyote.)
- 20 Akaendelea kusema, "Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia najisi.
- 21 Kwa maana kutoka ndani, katika moyo wa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji,
- 22 uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu.
- 23 Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu najisi."
- 24 Yesu aliondoka hapo, akaenda hadi wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha.
- 25 Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake.
- 26 Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu.
- 27 Yesu akamwambia, "Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa."
- 28 Lakini huyo mama akasema, "Sawa, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto."
- 29 Yesu akamwambia, "Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!"
- 30 Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka.
- 31 Kisha Yesu aliondoka wilayani Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli.
- 32 Basi, wakamletea bubu-kiziwi, wakamwomba amwekee mikono.
- 33 Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi.
- 34 Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, "Efatha," maana yake, "Funguka."
- 35 Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa.
- 36 Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo.
- 37 Watu walishangaa sana, wakasema, "Amefanya yote vyema: amewajalia viziwi kusikia, na bubu kusema!"