마가복음 9장 Swahili NT
- 1 Yesu akaendelea kuwaambia, "Kweli nawaambieni, wako wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu ukija kwa enzi."
- 2 Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane juu ya mlima mrefu peke yao. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao,
- 3 mavazi yake yakang'aa, yakawa meupe sana, jinsi dobi yeyote duniani asingeweza kuyafanya meupe.
- 4 Eliya na Mose wakawatokea, wakazungumza na Yesu.
- 5 Petro akamwambia Yesu, "Mwalimu, ni vizuri sana kwamba tuko hapa. Basi, afadhali tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya."
- 6 Yeye na wenzake waliogopa hata hakujua la kusema.
- 7 Kisha likatokea wingu likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu, "Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni."
- 8 Mara wanafunzi hao wakatazama tena, lakini hawakumwona mtu mwingine, ila Yesu peke yake pamoja nao.
- 9 Walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka kutoka wafu.
- 10 Basi, wakashika agizo hilo, lakini wakawa wanajadiliana wao kwa wao maana ya kufufuka kutoka wafu.
- 11 Wakamwuliza Yesu, "Mbona walimu wa Sheria wanasema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?"
- 12 Naye akawajibu, "Naam, Eliya anakuja kwanza kutayarisha yote. Hata hivyo, kwa nini basi imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Mwana wa Mtu atapatwa na mateso mengi na kudharauliwa?
- 13 Lakini nawaambieni, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyotaka kama ilivyoandikwa juu yake."
- 14 Walipowafikia wale wanafunzi wengine, waliona umati mkubwa wa watu hapo. Na baadhi ya walimu wa Sheria walikuwa wanajadiliana nao.
- 15 Mara tu ule umati wa watu ulipomwona, wote walishangaa sana, wakamkimbilia wamsalimu.
- 16 Yesu akawauliza, "Mnajadiliana nini nao?"
- 17 Hapo mtu mmoja katika ule umati wa watu akamjibu, "Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo aliyemfanya kuwa bubu.
- 18 Kila mara anapomvamia, humwangusha chini na kumfanya atokwe na povu kinywani, akisaga meno na kuwa mkavu mwili wote. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo lakini hawakuweza."
- 19 Yesu akawaambia, "Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kwangu."
- 20 Wakampeleka. Mara tu huyo pepo alipomwona Yesu, alimtia mtoto kifafa, naye mtoto akaanguka chini, akagaagaa na kutoka povu kinywani. Yesu akamwuliza baba yake huyo mtoto,
- 21 "Amepatwa na mambo hayo tangu lini?" Naye akamjibu, "Tangu utoto wake.
- 22 Na mara nyingi pepo huyo amemwangusha motoni na majini, ili amwangamize kabisa. Basi, ikiwa waweza, utuhurumie na kutusaidia!"
- 23 Yesu akamwambia, "Eti ikiwa waweza! Mambo yote yanawezekana kwa mtu aliye na imani."
- 24 Hapo, huyo baba akalia kwa sauti, "Naamini! Lakini imani yangu haitoshi, nisaidie!"
- 25 Yesu alipouona umati wa watu unaongezeka upesi mbele yake, alimkemea yule pepo mchafu, "Pepo unayemfanya huyu mtoto kuwa bubu-kiziwi, nakuamuru, mtoke mtoto huyu wala usimwingie tena!"
- 26 Hapo huyo pepo alipaaza sauti, akamwangusha huyo mtoto chini, kisha akamtoka. Mtoto alionekana kama maiti, hata wengine walisema, "Amekufa!"
- 27 Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.
- 28 Yesu alipoingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza kwa faragha, "Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?"
- 29 Naye akawaambia, "Pepo wa aina hii hawezi kutoka isipokuwa kwa sala tu."
- 30 Yesu na wanafunzi wake waliondoka hapo, wakaendelea na safari kupitia wilaya ya Galilaya. Yesu hakupenda watu wajue alipokuwa,
- 31 kwa sababu alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Aliwaambia, "Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu ambao watamuua; lakini siku ya tatu baada ya kuuawa atafufuka."
- 32 Wanafunzi hawakufahamu jambo hilo. Wakaogopa kumwuliza.
- 33 Basi, walifika Kafarnaumu. Na alipokuwa nyumbani, aliwauliza, "Mlikuwa mnajadiliana nini njiani?"
- 34 Lakini wao wakanyamaza, maana njiani walikuwa wamebishana ni nani aliye mkuu kati yao.
- 35 Yesu akaketi chini, akawaita wale kumi na wawili, akawaambia, "Yeyote anayetaka kuwa wa kwanza lazima awe wa mwisho na kuwa mtumishi wa wote."
- 36 Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kati yao, akamku mbatia, halafu akawaambia,
- 37 "Anayempokea mtoto kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, hanipokei mimi tu, bali anampokea yule aliyenituma."
- 38 Yohane akamwambia, "Mwalimu, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako, nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu."
- 39 Lakini Yesu akasema, "Msimkataze, maana hakuna mtu anayefanya muujiza kwa jina langu, na papo hapo akaweza kusema mabaya juu yangu.
- 40 Maana, asiyepingana nasi, yuko upande wetu.
- 41 Mtu yeyote atakeyewapeni kikombe cha maji ya kunywa kwa sababu ninyi ni watu wake Kristo, hakika hatakosa kupata tuzo lake.
- 42 "Mtu yeyote atakayemfanya mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini atende dhambi, ingekuwa afadhali kwa mtu huyo kufungiwa shingoni mwake jiwe kubwa la kusagia na kutupwa baharini.
- 43 Mkono wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia kwenye uzima bila mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili na kwenda katika moto wa Jehanamu.
- 44 Humo, wadudu wake hawafi na moto hauzimiki.
- 45 Na mguu wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia katika uzima bila mguu mmoja, kuliko kuwa na miguu yote miwili na kutupwa katika moto wa Jehanamu.
- 46 Humo, wadudu wake hawafi na moto hauzimiki.
- 47 Na jicho lako likikukosesha, ling'oe! Afadhali kuingia katika utawala wa Mungu ukiwa na jicho moja tu, kuliko kuwa na macho yako yote mawili na kutupwa katika moto wa Jehanamu.
- 48 Humo wadudu wake hawafi, na moto hauzimiki.
- 49 "Maana kila mmoja atakolezwa kwa moto.
- 50 Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini? Muwe na chumvi ndani yenu na kudumisha amani kati yenu."