누가복음 15장 Swahili NT
- 1 Siku moja, watoza ushuru na wahalifu wengi walikwenda kumsikiliza Yesu.
- 2 Mafarisayo na walimu wa Sheria wakaanza kunung'unika: "Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao."
- 3 Yesu akawajibu kwa mfano:
- 4 "Hivi, mtu akiwa na kondoo mia, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, atafanya nini? Atawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate.
- 5 Akimpata, atambeba mabegani kwa furaha.
- 6 Anapofika nyumbani, atawaita rafiki zake akiwaambia, Furahini pamoja nami, kwa sababu nimempata yule kondoo wangu aliyepotea.
- 7 Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu.
- 8 "Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, aifagie nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate.
- 9 Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake akisema, Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.
- 10 Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu."
- 11 Yesu akaendelea kusema, "Kulikuwa na mtu mmoja mwenye wana wawili.
- 12 Yule mdogo, alimwambia baba yake: Baba, nipe urithi wangu. Naye akawagawia mali yake.
- 13 Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo.
- 14 Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika.
- 15 Akaomba kazi kwa mwananchi mtu mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe.
- 16 Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu.
- 17 Alipoanza kupata akili akafikiri: Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa?
- 18 Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia.
- 19 Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.
- 20 Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu.
- 21 "Mwanawe akamwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.
- 22 Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu!
- 23 Mchinjeni ndama mnono; tule kusherehekea!
- 24 Kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa, kumbe yu mzima alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana. Wakaanza kufanya sherehe.
- 25 "Wakati huo kaka yake alikuwa bado shambani. Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumbani akasikia vifijo na ngoma.
- 26 Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza: Kuna nini?
- 27 Huyo mtumishi akamwambia: Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.
- 28 Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie.
- 29 Lakini yeye akamjibu: Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwana mbuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu!
- 30 Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.
- 31 Baba yake akamjibu: Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako.
- 32 Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana."