누가복음 2장 Swahili NT
- 1 Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote chini ya utawala wake wajiandikishe.
- 2 Kuandikishwa huku kulikuwa mara ya kwanza, wakati Kirenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria.
- 3 Basi, wote waliohusika walikwenda kujiandikisha, kila mtu katika mji wake.
- 4 Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya. Kwa kuwa alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yuda alikozaliwa Mfalme Daudi.
- 5 Alikwenda kujiandikisha pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mja mzito.
- 6 Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia,
- 7 akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.
- 8 Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao.
- 9 Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana.
- 10 Malaika akawaambia, "Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kuu kwa watu wote.
- 11 Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana.
- 12 Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini."
- 13 Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema:
- 14 "Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu aliopendezwa nao!"
- 15 Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: "Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha."
- 16 Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini.
- 17 Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake.
- 18 Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji.
- 19 Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake.
- 20 Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa.
- 21 Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.
- 22 Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na Sheria ya Mose, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele ya Bwana.
- 23 Katika Sheria ya Bwana imeandikwa: "Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana."
- 24 Pia walikwenda ili watoe sadaka: hua wawili au makinda wawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Bwana.
- 25 Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye.
- 26 Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Masiha wa Bwana.
- 27 Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia Hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta Hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na Sheria,
- 28 Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu na kusema:
- 29 "Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani.
- 30 Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu utokao kwako,
- 31 ambao umeutayarisha mbele ya watu wote:
- 32 Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli."
- 33 Baba na mama yake Yesu walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto.
- 34 Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, "Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu;
- 35 na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako."
- 36 Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa.
- 37 Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa Hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana.
- 38 Saa hiyohiyo alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na akaeleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu.
- 39 Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na Sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, mkoani Galilaya.
- 40 Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa pamoja naye.
- 41 Wazazi wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka.
- 42 Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi.
- 43 Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari.
- 44 Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki.
- 45 Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta.
- 46 Siku ya tatu walimkuta Hekaluni kati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.
- 47 Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima.
- 48 Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, "Mwanangu, kwa nini umetutenda hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni."
- 49 Yeye akawajibu, "Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?"
- 50 Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia.
- 51 Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake.
- 52 Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.