누가복음 21장 Swahili NT
- 1 Yesu alitazama kwa makini, akawaona matajiri walivyokuwa wanatia sadaka zao katika hazina ya Hekalu,
- 2 akamwona pia mama mmoja mjane akitumbukiza humo sarafu mbili ndogo.
- 3 Basi, akasema, "Nawaambieni kweli, mama huyu mjane ametia zaidi katika hazina kuliko wote.
- 4 Kwa maana, wengine wote wametoa sadaka zao kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi."
- 5 Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanazungumza juu ya Hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe ya thamani, pamoja na sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Yesu akasema,
- 6 "Haya yote mnayoyaona--zitakuja siku ambapo hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa."
- 7 Basi, wakamwuliza, "Mwalimu, mambo hayo yatatokea lini? Na ni ishara gani zitakazoonyesha kwamba karibu mambo hayo yatokee?"
- 8 Yesu akawajibu, "Jihadharini, msije mkadanganyika. Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: Mimi ndiye, na, Wakati ule umekaribia. Lakini ninyi msiwafuate!
- 9 Basi, mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msitishike; maana ni lazima hayo yatokee kwanza, lakini mwisho wa yote, bado."
- 10 Halafu akaendelea kusema: "Taifa moja litapigana na taifa lingine, na ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine.
- 11 Kila mahali kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, kutakuwa na njaa na tauni. Kutakuwa na vituko vya kutisha na ishara kubwa angani.
- 12 Lakini kabla ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu.
- 13 Hii itawapeni fursa ya kushuhudia Habari Njema.
- 14 Muwe na msimamo huu mioyoni mwenu: hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi mtakavyojitetea,
- 15 kwa sababu mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hivyo kwamba zenu hawataweza kustahimili wala kupinga.
- 16 Wazazi wenu, ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti ninyi; na baadhi yenu mtauawa.
- 17 Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu.
- 18 Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea.
- 19 Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu.
- 20 "Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo mtambue ya kwamba wakati umefika ambapo mji huo utaharibiwa.
- 21 Hapo walioko Yudea wakimbilie milimani; wale walio mjini watoke; na wale walio mashambani wasirudi mjini.
- 22 Kwa maana siku hizo ni siku za adhabu, ili yote yaliyoandikwa yatimie.
- 23 Ole wao waja wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa.
- 24 Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia.
- 25 "Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari.
- 26 Watu watazirai kwa sababu ya uoga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa.
- 27 Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi.
- 28 Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia."
- 29 Kisha akawaambia mfano: "Angalieni mtini na miti mingine yote.
- 30 Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
- 31 Vivyo hivyo, mtakapoona mambo hayo yanatendeka, mtatambua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.
- 32 Nawaambieni hakika, kizazi hiki cha sasa hakitapita kabla ya hayo yote kutendeka.
- 33 Mbingu na dunia vitapita, lakini maneno yangu hayatapita.
- 34 "Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, Siku ile itawajieni ghafla.
- 35 Kwa maana itawajia kama mtego, wote wanaoishi duniani pote.
- 36 Muwe waangalifu basi, na salini daima ili muweze kupata nguvu ya kupita salama katika mambo haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele ya Mwana wa Mtu."
- 37 Wakati wa mchana, siku hizo, Yesu alikuwa akifundisha watu Hekaluni; lakini usiku alikuwa akienda katika mlima wa Mizeituni na kukaa huko.
- 38 Watu wote walikuwa wanakwenda Hekaluni asubuhi na mapema, wapate kumsikiliza.