누가복음 24장 Swahili NT
- 1 Jumapili, alfajiri na mapema, wale wanawake walikwenda kaburini wakichukua yale manukato waliyotayarisha.
- 2 Walikuta lile jiwe limeviringishwa mbali na kaburi.
- 3 Walipoingia ndani, hawakuona mwili wa Bwana Yesu.
- 4 Walipokuwa bado wanashangaa juu ya jambo hilo, mara watu wawili waliovaa mavazi yenye kung'aa sana, wakasimama karibu nao.
- 5 Hao wanawake wakaingiwa na hofu, wakainama chini. Ndipo wale watu wakawaambia, "Kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu?
- 6 Hayuko hapa; amefufuka. Kumbukeni aliyowaambieni alipokuwa kule Galilaya:
- 7 Ni lazima Mwana wa Mtu atolewe kwa watu waovu, nao watamsulubisha, na siku ya tatu atafufuka."
- 8 Hapo wanawake wakayakumbuka maneno yake,
- 9 wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja na wengine habari za mambo hayo yote.
- 10 Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene, Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao.
- 11 Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi, hivyo hawakuamini.
- 12 Lakini Petro alitoka, akaenda mbio hadi kaburini. Alipoinama kuchungulia ndani, akaiona tu ile sanda. Akarudi nyumbani huku akiwa anashangaa juu ya hayo yaliyotokea.
- 13 Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu.
- 14 Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia.
- 15 Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao.
- 16 Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua.
- 17 Akawauliza, "Mnazungumza nini huku mnatembea?" Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni.
- 18 Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, "Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?"
- 19 Naye akawajibu, "Mambo gani?" Wao wakamjibu, "Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote.
- 20 Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha.
- 21 Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka.
- 22 Tena, wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi,
- 23 wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika waliowaambia kwamba alikuwa hai.
- 24 Wengine wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye hawakumwona."
- 25 Kisha Yesu akawaambia, "Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii?
- 26 Je, haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?"
- 27 Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote.
- 28 Walipokikaribia kile kijiji walikokuwa wanakwenda, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari;
- 29 lakini wao wakamsihi wakisema, "Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia." Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao.
- 30 Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.
- 31 Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao.
- 32 Basi, wakaambiana, "Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?"
- 33 Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu: wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika
- 34 wakisema, "Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni."
- 35 Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate.
- 36 Wanafunzi wote wawili walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia "Amani kwenu."
- 37 Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu.
- 38 Lakini yeye akawaambia, "Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni mwenu?
- 39 Angalieni mikono na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni mkanione, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo."
- 40 Baada ya kusema hayo, akawaonyesha mikono na miguu.
- 41 Wakiwa bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa wanastaajabu, akawauliza, "Mnacho chakula chochote hapa?"
- 42 Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa.
- 43 Akakichukua, akala, wote wakimwona.
- 44 Halafu akawaambia, "Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi: kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote yaliyoandikwa juu yangu katika Sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi."
- 45 Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu.
- 46 Akawaambia, "Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka wafu,
- 47 na kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia na Yerusalemu yahubiriwe juu ya kutubu na kusamehewa dhambi.
- 48 Ninyi ni mashahidi wa mambo hayo.
- 49 Nami mwenyewe nitawapelekeeni yule ambaye Baba aliahidi kumtuma, lakini ngojeni huku mjini mpaka mtakapopewa ile nguvu itokayo juu."
- 50 Kisha akawaongoza nje ya mji hadi Bethania, akainua mikono yake juu, akawabariki.
- 51 Alipokuwa anawabariki, akawaacha; akachukuliwa mbinguni.
- 52 Wao wakamwabudu, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kubwa:
- 53 wakakaa muda wote Hekaluni wakimsifu Mungu.