누가복음 4장 Swahili NT
- 1 Yesu alitoka katika mto Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani.
- 2 Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa.
- 3 Ndipo Ibilisi akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate."
- 4 Yesu akamjibu, "Imeandikwa: Mtu haishi kwa mkate tu."
- 5 Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonyesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia,
- 6 "Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza.
- 7 Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu."
- 8 Yesu akamjibu, "Imeandikwa: Utamwabudu Bwana Mungu wako, na utamtumikia yeye peke yake."
- 9 Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa Hekalu, akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu,
- 10 kwa maana imeandikwa: Atawaamuru malaika wake wakulinde,
- 11 na tena, Watakuchukua mikononi mwao usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe."
- 12 Lakini Yesu akamjibu, "Imeandikwa: Usimjaribu Bwana Mungu wako."
- 13 Ibilisi alipokwishamjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda.
- 14 Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani.
- 15 Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote.
- 16 Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi, kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti.
- 17 Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa:
- 18 "Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani amenipaka mafuta niwahubirie maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa,
- 19 na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana."
- 20 Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho.
- 21 Naye akaanza kuwaambia, "Andiko hili mlilosikia likisomwa, limetimia leo."
- 22 Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakanena, "Je, huyu si mwana wa Yosefu?"
- 23 Naye akawaambia, "Bila shaka mtaniambia msemo huu: Mganga jiponye mwenyewe, na pia mtasema: Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye hapa pia katika kijiji chako."
- 24 Akaendelea kusema, "Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi katika kijiji chake.
- 25 Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Eliya. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote.
- 26 Hata hivyo, Eliya hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarepta, Sidoni.
- 27 Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani, mwenyeji wa Siria."
- 28 Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana.
- 29 Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini.
- 30 Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.
- 31 Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu katika mkoa wa Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato.
- 32 Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha.
- 33 Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na roho ya pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio:
- 34 "We! Yesu wa Nazareti! Kwa nini unatuingilia? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni mjumbe Mtakatifu wa Mungu!"
- 35 Lakini Yesu akamkemea huyo pepo akisema: "Nyamaza! Mtoke mtu huyu!" Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo.
- 36 Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, "Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!"
- 37 Habari zake zikaenea mahali pote katika mkoa ule.
- 38 Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye.
- 39 Yesu akaenda akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Mara yule mama akainuka, akawatumikia.
- 40 Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote.
- 41 Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: "Wewe u Mwana wa Mungu!" Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walimfahamu kwamba yeye ndiye Kristo.
- 42 Kesho yake asubuhi Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta, na walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao.
- 43 Lakini yeye akawaambia, "Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo."
- 44 Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea.