요한복음 10장 Swahili NT
- 1 Yesu alisema "Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang'anyi.
- 2 Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo.
- 3 Mngoja mlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake, naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake na kuwaongoza nje.
- 4 Akisha watoa nje huwatangulia mbele nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake.
- 5 Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake."
- 6 Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia.
- 7 Basi, akasema tena, "Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo.
- 8 Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyang'anyi, nao kondoo hawakuwasikiliza.
- 9 Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho.
- 10 Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uzima--uzima kamili.
- 11 "Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake.
- 12 Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwa mwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia. Kisha mbwa mwitu huwakamata na kuwatawanya.
- 13 Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu.
- 14 Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi,
- 15 kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao.
- 16 Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.
- 17 "Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena.
- 18 Hakuna mtu anayeninyang'anya uhai wangu; mimi na nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye."
- 19 Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya.
- 20 Wengi wao wakasema, "Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?"
- 21 Wengine wakasema, "Haya si maneno ya mwenye pepo. Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?"
- 22 Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya Kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi.
- 23 Naye Yesu akawa anatembea Hekaluni katika ukumbi wa Solomoni.
- 24 Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, "Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo, basi, tuambie wazi."
- 25 Yesu akawajibu, "Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia.
- 26 Lakini ninyi hamsadiki kwa sababu ninyi si kondoo wangu.
- 27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata.
- 28 Mimi nawapa uzima wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu.
- 29 Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wale hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba.
- 30 Mimi na Baba, tu mmoja."
- 31 Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie.
- 32 Yesu akawaambia, "Nimewaonyesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?"
- 33 Wayahudi wakamjibu, "Hatukupigi mawe kwa ajili ya tendo jema, ila kwa sababu ya kukufuru! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu."
- 34 Yesu akawajibu, "Je, haikuandikwa katika Sheria yenu: Mimi nimesema, ninyi ni miungu?
- 35 Mungu aliwaita miungu wale waliopewa neno lake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima.
- 36 Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: Unakufuru, eti kwa sababu nilisema: Mimi ni Mwana wa Mungu?
- 37 Kama sifanyi kazi za Baba yangu msiniamini.
- 38 Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake."
- 39 Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao.
- 40 Yesu akaenda tena ng'ambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko.
- 41 Watu wengi walimwendea wakasema, "Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa."
- 42 Watu wengi mahali hapo wakamwamini.