요한복음 12장 Swahili NT
- 1 Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika Bethania alikoishi Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu.
- 2 Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu.
- 3 Basi, Maria alichukua chupa ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi.
- 4 Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema,
- 5 "Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari mia tatu, wakapewa maskini?"
- 6 Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina.
- 7 Lakini Yesu akasema, "Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu.
- 8 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote."
- 9 Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu.
- 10 Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro,
- 11 Maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu.
- 12 Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu.
- 13 Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaaza sauti wakisema: "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli."
- 14 Yesu akampata mwana punda mmoja akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko:
- 15 "Usiogope mji wa Sioni! Tazama, Mfalme wako anakuja, Amepanda mwana punda."
- 16 Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo.
- 17 Kundi la watu wale waliokuwa pamoja naye wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka wafu, walisema yaliyotukia.
- 18 Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo.
- 19 Basi, Mafarisayo wakaambiana, "Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata."
- 20 Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo.
- 21 Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, "Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu."
- 22 Filipo akaenda akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu.
- 23 Yesu akawaambia, "Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika!
- 24 Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi.
- 25 Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uzima wa milele.
- 26 Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima.
- 27 "Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: Baba, usiruhusu saa hii inifikie? Lakini ndiyo maana nimekuja--ili nipite katika saa hii.
- 28 Baba, ulitukuze jina lako." Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, "Nimelitukuza, na nitalitukuza tena."
- 29 Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, "Malaika ameongea naye!"
- 30 Lakini Yesu akawaambia, "Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu.
- 31 Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa.
- 32 Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu."
- 33 (Kwa kusema hivyo alionyesha atakufa kifo gani).
- 34 Basi, umati huo ukamjibu, "Sisi tunaambiwa na Sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?"
- 35 Yesu akawaambia, "Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako.
- 36 Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga." Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao.
- 37 Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini.
- 38 Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: "Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?"
- 39 Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya tena alisema:
- 40 "Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili zao; wasione kwa macho yao, wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema Bwana, ili nipate kuwaponya."
- 41 Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake.
- 42 Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi.
- 43 Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu
- 44 Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, "Mtu aliyeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma.
- 45 Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma.
- 46 Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani.
- 47 Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki mimi sitamhukumu; maana sikuja kuhukumu ulimwengu bali kuuokoa.
- 48 Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho.
- 49 Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini.
- 50 Nami najua kuwa amri yake huleta uzima wa milele. Basi, mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme."