사도행전 11장 Swahili NT
- 1 Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu.
- 2 Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waumini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu wakisema:
- 3 "Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula pamoja nao!
- 4 Hapo Petro akawaeleza kinaganaga juu ya yale yaliyotendeka tangu mwanzo:
- 5 "Siku moja nikiwa nasali mjini Yopa, niliona maono; niliona kitu kama shuka kubwa likishushwa chini kutoka mbinguni likiwa limeshikwa pembe zake nne, likawekwa kando yangu.
- 6 Nilichungulia ndani kwa makini nikaona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani.
- 7 Kisha nikasikia sauti ikiniambia: Petro amka, chinja, ule.
- 8 Lakini mimi nikasema: La, Bwana; maana chochote kilicho najisi au kichafu hakijapata kamwe kuingia kinywani mwangu.
- 9 Ile sauti ikasikika tena kutoka mbinguni: Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa.
- 10 Jambo hilo lilifanyika mara tatu, na mwishowe vyote vilirudishwa juu mbinguni.
- 11 Ghafla, watu watatu waliokuwa wametumwa kwangu kutoka Kaisarea waliwasili kwenye nyumba niliyokuwa nakaa.
- 12 Roho aliniambia niende pamoja nao bila kusita. Hawa ndugu sita waliandamana nami pia kwenda Kaisarea na huko tuliingia nyumbani mwa Kornelio.
- 13 Yeye alitueleza jinsi alivyokuwa amemwona malaika amesimama nyumbani mwake na kumwambia: Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro.
- 14 Yeye atakuambia maneno ambayo kwayo wewe na jamaa yako yote mtaokolewa.
- 15 Na nilipoanza tu kuongea, Roho Mtakatifu aliwashukia kama alivyotushukia sisi pale awali.
- 16 Hapo nilikumbuka yale maneno Bwana aliyosema: Yohane alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.
- 17 Basi, kama Mungu amewapa pia watu wa mataifa mengine zawadi ileile aliyotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu Kristo, je, mimi ni nani hata nijaribu kumpinga Mungu?"
- 18 Waliposikia hayo, waliacha ubishi, wakamtukuza Mungu wakisema, "Mungu amewapa watu wa mataifa mengine nafasi ya kutubu na kuwa na uzima!"
- 19 Kutokana na mateso yaliyotokea wakati Stefano alipouawa, waumini walitawanyika. Wengine walikwenda mpaka Foinike, Kupro na Antiokia wakihubiri ule ujumbe kwa Wayahudi tu.
- 20 Lakini baadhi ya waumini waliotoka Kupro na Kurene, walikwenda Antiokia wakautangaza huo ujumbe kwa watu wa mataifa mengine wakiwahubiria ile Habari Njema juu ya Bwana Yesu.
- 21 Bwana aliwasaidia na idadi kubwa ya watu iliamini na kumgeukia Bwana.
- 22 Habari ya jambo hilo ikasikika kwa lile kanisa la Yerusalemu. Hivyo wakamtuma Barnaba aende Antiokia.
- 23 Alipofika huko na kuona jinsi Mungu alivyowaneemesha wale watu, alifurahi na kuwahimiza wote wadumu katika uaminifu wao kwa Bwana.
- 24 Barnaba alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana.
- 25 Kisha, Barnaba alikwenda Tarso kumtafuta Saulo
- 26 Alipompata, alimleta Antiokia. Nao wote wawili walikaa na lile kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antiokia, ndiko, kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo.
- 27 Wakati huohuo, manabii kadhaa walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu.
- 28 Basi, mmoja wao aitwaye Agabo alisimama, na kwa uwezo wa Roho akabashiri kwamba kutakuwa na njaa kubwa katika nchi yote (Njaa hiyo ilitokea wakati Klaudio alipokuwa akitawala).
- 29 Wale wanafunzi waliamua kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake apeleke chochote ili kuwasaidia wale ndugu waliokuwa wanaishi Yudea.
- 30 Basi, wakafanya hivyo na kupeleka mchango wao kwa wazee wa kanisa kwa mikono ya Barnaba na Saulo.