사도행전 1장 Swahili NT
- 1 Ndugu Theofilo, Katika kitabu cha kwanza niliandika juu ya mambo yote Yesu aliyotenda na kufundisha tangu mwanzo wa kazi yake
- 2 mpaka siku ile alipochukuliwa mbinguni. Kabla ya kuchukuliwa mbinguni aliwapa maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua.
- 3 Kwa muda wa siku arobaini baada ya kifo chake aliwatokea mara nyingi kwa namna ambazo zilithibitisha kabisa kwamba alikuwa hai. Walimwona, naye aliongea nao juu ya ufalme wa Mungu.
- 4 Wakati walipokutana pamoja aliwaamuru hivi: "Msiondoke Yerusalemu, bali ngojeeni ile zawadi aliyoahidi Baba, zawadi ambayo mlikwisha nisikia nikiongea juu yake.
- 5 Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache, ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu."
- 6 Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, "Je Bwana, wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?"
- 7 Lakini Yesu akawaambia, "Nyakati na majira ya mambo hayo viko chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini.
- 8 Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni ninyi, mtajazwa nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia."
- 9 Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena.
- 10 Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao,
- 11 wakasema, "Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni atakuja tena namna hiyohiyo mliivyomwona akienda mbinguni."
- 12 Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka mlima wa Mizeituni ulioko karibu kilomita moja kutoka mjini.
- 13 Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo.
- 14 Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake.
- 15 Siku chache baadaye, kulikuwa na mkutano wa waumini, karibu watu mia moja na ishirini. Petro alisimama mbele yao,
- 16 akasema, "Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi, alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu nguvuni.
- 17 Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu maana alichaguliwa ashiriki huduma yetu.
- 18 ("Mnajua kwamba yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na kitendo chake kiovu. Akaanguka chini, akapasuka na matumbo yake yakamwagika nje.
- 19 Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba Hekeli Dama, maana yake, Shamba la Damu.)
- 20 Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi: Nyumba yake ibaki mahame; mtu yeyote asiishi ndani yake. Tena imeandikwa: Mtu mwingine achukue nafasi yake katika huduma hiyo.
- 21 Kwa hiyo, ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi kama shahidi wa ufufuo wake Bwana Yesu.
- 22 Anapaswa kuwa mmoja wa wale waliokuwa katika kundi letu wakati wote Bwana alipokuwa anasafiri pamoja nasi, tangu wakati Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa kutoka kwetu kwenda mbinguni."
- 23 Basi, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia.
- 24 Kisha wakasali: "Bwana, wewe unajua mioyo ya watu wote. Hivyo, utuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua
- 25 ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda mahali pake mwenyewe."
- 26 Hapo, wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja.