로마서 12장 Swahili NT
- 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, maadam Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: jitoleeni nafsi zenu kwa Mungu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu.
- 2 Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu, kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu.
- 3 Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni ninyi nyote: msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kufuatana na kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja.
- 4 Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake.
- 5 Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.
- 6 Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kufuatana na neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake.
- 7 Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe.
- 8 Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha.
- 9 Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema.
- 10 Pendaneni kidugu; kila mmoja amfikirie mwenzake kwanza kwa heshima.
- 11 Msilegee katika bidii, muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana.
- 12 Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida na kusali daima.
- 13 Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu.
- 14 Watakieni baraka wote wanaowadhulumu ninyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani.
- 15 Furahini pamoja na wanaofurahi, lieni pamoja na wanaolia.
- 16 Muwe na wema uleule kwa kila mtu. Msijitakie makuu, bali jishugulisheni na watu wadogo. Msijione kuwa wenye hekima sana.
- 17 Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote.
- 18 Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote.
- 19 Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza asema Bwana."
- 20 Tena, Maandiko yasema: "Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake."
- 21 Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.