로마서 9장 Swahili NT
- 1 Nasema ukweli mtupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo. Dhamiri yangu ikiongozwa na Roho Mtakatifu inanithibitishia jambo hili pia.
- 2 Nataka kusema hivi: nina huzuni kubwa na maumivu yasiyopimika moyoni mwangu
- 3 kwa ajili ya watu wangu, walio damu moja nami! Kama ingekuwa kwa faida yao, ningekuwa radhi kulaaniwa na kutengwa na Kristo.
- 4 Hao ndio watu wa Israeli ambao Mungu aliwateua wawe watoto wake, akawashirikisha utukufu wake; aliagana nao, akawapa Sheria yake, imani ya kweli na ahadi zake.
- 5 Wao ni wajukuu wa mababu, naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao. Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele! Amina.
- 6 Sisemi kwamba ahadi ya Mungu imebatilika; maana si watu wote wa Israeli ni wateule wa Mungu.
- 7 Wala, si wazawa wote wa Abrahamu ni watoto wake wa kweli. Ila, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Wazao wake watatokana na Isaka."
- 8 Nido kusema, wale waliozaliwa kimaumbile ndio watoto wa Mungu, bali wale waliozaliwa kutokana na ahadi ya Mungu ndio watakaoitwa watoto wake.
- 9 Maana ahadi yenyewe ni hii: "Nitakujia wakati maalum, naye Sara atapata mtoto."
- 10 Tena si hayo tu ila pia Rebeka naye alipata mapacha kwa baba mmoja, yaani Isaka, babu yetu.
- 11 Lakini, ili Mungu aonekane kwamba anao uhuru wa kuchagua, hata kabla wale ndugu hawajazaliwa na kabla hawajaweza kupambanua jema na baya,
- 12 Rebeka aliambiwa kwamba yule mtoto wa kwanza atamtumikia yule wa nyuma. Hivyo uchaguzi wa Mungu unategemea jinsi anavyoita mwenyewe, na si matendo ya binadamu.
- 13 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Yakobo nilimpenda, lakini Esau nilimchukia."
- 14 Basi, tuseme nini? Je, Mungu amekosa haki? Hata kidogo!
- 15 Maana alimwambia Mose: "Nitamhurumia mtu yeyote ninayetaka kumhurumia; nitamwonea huruma mtu yeyote ninayetaka."
- 16 Kwa hiyo, yote hutegemea huruma ya Mungu, na si bidii au mapenzi ya mtu.
- 17 Maana Maandiko Matakatifu yasema hivi kwa Farao: "Nilikufanya mfalme ili kwa njia yako, uwezo wangu ujulikane, na jina langu litangazwe popote duniani."
- 18 Ni wazi, basi, kwamba Mungu humhurumia yeyote anayetaka kumhurumia, na akipenda kumfanya mtu awe mkaidi, hufanya hivyo.
- 19 Labda utaniuliza: "Ikiwa mambo yako hivyo, Mungu anawezaje kumlaumu mtu? Nani awezaye kuyapinga mapenzi yake?"
- 20 Lakini, ewe binadamu, u nani hata uthubutu kumhoji Mungu? Je, chungu chaweza kumwuliza mfinyanzi wake: "Kwa nini umenitengeneza namna hii?"
- 21 Mfinyanzi anaweza kuutumia udongo apendavyo na kufinyanga vyungu viwili kwa udongo uleule; kimoja kwa matumizi ya heshima, na kingine kwa matumizi ya kawaida.
- 22 Hivyo ndivyo ilivyo kwa Mungu. Alitaka kuonyesha ghadhabu yake na kujulisha uwezo wake, Basi, alikuwa na saburi sana, akiwavumilia wale ambao walikuwa lengo la ghadhabu yake, ambao walistahili kuangamizwa.
- 23 Alitaka pia kudhihirisha wingi wa utukufu wake ambao alitumiminia sisi tulio lengo la huruma yake; sisi ambao alikwisha kututayarisha kuupokea utukufu wake.
- 24 Maana sisi ndio hao aliowaita, si tu kutoka miongoni mwa Wayahudi bali pia kutoka kwa watu wa mataifa mengine.
- 25 Maana ndivyo asemavyo katika kitabu cha Hosea: "Wale waliokuwa Si watu wangu nitawaita: Watu wangu! Naye Sikupendi ataitwa: Mpenzi wangu!
- 26 Na pale walipoambiwa: Ninyi si wangu hapo wataitwa: Watoto wa Mungu hai."
- 27 Naye nabii Isaya, kuhusu Israeli anapaaza sauti: "Hata kama watoto wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaookolewa;
- 28 maana, Bwana ataitekeleza upesi hukumu yake kamili juu ya ulimwengu wote."
- 29 Ni kama Isaya alivyosema hapo awali: "Kama Bwana Mwenye Nguvu asingalituachia baadhi ya watoto wa Israeli, tungalikwisha kuwa kama Sodoma, tungalikwisha kuwa ma Gomora."
- 30 Basi, tuseme nini? Ni hivi: watu wa mataifa ambao hawakutafuta kukubaliwa kuwa waadilifu, wamekubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani,
- 31 hali watu wa Israeli waliokuwa wakitafuta Sheria iletayo kukubaliwa kuwa waadilifu, hawakuipata.
- 32 Kwa nini? Kwa sababu walitegemea matendo yao badala ya kutegemea imani. Walijikwaa juu ya jiwe la kujikwaa
- 33 kama yesemavyo Maandiko Matakatifu: "Tazama! Naweka huko Sioni jiwe likwazalo, mwamba utakaowafanya watu waanguke. Mtu atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa!"