고린도전서 16장 Swahili NT
- 1 Sasa, yahusu ule mchango kwa ajili ya watu wa Mungu: fanyeni kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia.
- 2 Kila Jumapili kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha kadiri ya mapato yake, ili kusiwe na haja ya kufanya mchango wakati nitakapokuja.
- 3 Wakati nitakapokuja kwenu, nitawatuma wale mtakaowachagua miongoni mwenu wapeleke barua na zawadi zenu Yerusalemu.
- 4 Kama itafaa nami niende, basi, watakwenda pamoja nami.
- 5 Nitakuja kwenu, baada ya kupitia Makedonia--maana nataraji kupitia Makedonia.
- 6 Labda nitakaa kwenu kwa muda fulani, au huenda nitakaa pamoja nanyi wakati wote wa baridi, ili mpate kunisaidia niendelee na safari yangu kokote nitakakokwenda.
- 7 Sipendi kupita kwenu harakaharaka na kuendelea na safari. Natumaini kukaa kwenu kwa kitambo fulani, Bwana akiniruhusu.
- 8 Lakini nitabaki hapa Efeso mpaka siku ya Pentekoste.
- 9 Mlango uko wazi kabisa kwa ajili ya kazi yangu muhimu hapa, ingawa wapinzani nao ni wengi.
- 10 Timotheo akija, angalieni asiwe na hofu yoyote wakati yupo kati yenu, kwani anafanya kazi ya Bwana kama mimi.
- 11 Kwa hiyo mtu yeyote asimdharau, ila msaidieni aendelee na safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu, maana mimi namngojea pamoja na ndugu zetu.
- 12 Kuhusu ndugu Apolo, nimemsihi sana aje kwenu pamoja na ndugu wengine, lakini hapendelei kabisa kuja sasa ila atakuja mara itakapowezekana.
- 13 Kesheni, simameni imara katika imani, muwe hodari na wenye nguvu.
- 14 Kila mfanyacho kifanyike kwa upendo.
- 15 Ndugu, mnaifahamu jamaa ya Stefana; wao ni watu wa kwanza kabisa kuipokea imani ya Kikristo katika Akaya, na wamejitolea kuwatumikia watu wa Mungu. Ninawasihi ninyi ndugu zangu,
- 16 muufuate uongozi wa watu kama hao, na uongozi wa kila mtu afanyaye kazi na kutumikia pamoja nao.
- 17 Nafurahi sana kwamba Stefana, Fortunato na Akaiko wamefika; wamelijaza pengo lililokuwako kwa kutokuwako kwenu.
- 18 Wameiburudisha roho yangu na yenu pia. Kwa hiyo inafaa kuwakumbuka watu wa namna hii.
- 19 Makanisa yote ya Asia yanawasalimuni. Akula na Priskila pamoja na watu wote wa Mungu walio nyumbani mwao wanawasalimuni sana katika Bwana.
- 20 Ndugu wote wanawasalimuni. Nanyi salimianeni kwa ishara ya mapendo ya Mungu.
- 21 Mimi Paulo nawasalimuni, nikiandika kwa mkono wangu mwenyewe.
- 22 Yeyote asiyempenda Bwana, na alaaniwe. MARANA THA--BWANA, njoo!
- 23 Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi.
- 24 Mapendo yangu yawe kwenu katika kuungana na Kristo Yesu.