고린도전서 2장 Swahili NT
- 1 Ndugu, mimi nilipokuja kwenu sikuwahubiria siri ya ujumbe wa Mungu kwa ufasaha wa lugha, au kwa hekima ya binadamu.
- 2 Nilipokuwa kwenu niliamua kutojua chochote kile isipokuwa tu kumjua Yesu Kristo; naam, Kristo aliyesulubiwa.
- 3 Nilipokuwa kwenu nilikuwa dhaifu, natetemeka kwa hofu nyingi.
- 4 Hotuba zangu na mahubiri yangu sikuyatoa kwa maneno ya kuvutia na ya hekima, bali kwa uthibitisho mwingi na nguvu ya Roho.
- 5 Nilifanya hivyo kusudi imani yenu ipate kutegemea nguvu ya Mungu, na si hekima ya binadamu.
- 6 Hata hivyo, sisi tunatumia lugha ya hekima kwa wale waliokomaa kiroho; lakini hekima hiyo si ya hapa duniani, wala si ya watawala wa dunia hii ambao wako katika mkumbo wa kupotea.
- 7 Hekima tunayotumia ni hekima ya siri ya Mungu, hekima iliyofichika, ambayo Mungu aliiazimia tangu mwanzo kwa ajili ya utukufu wetu.
- 8 Ni hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana wangalielewa, hawangalimsulubisha Bwana wa utukufu.
- 9 Lakini, ni kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona wala sikio kuyasikia, mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao."
- 10 Hayo ndiyo mambo Mungu aliyotufunulia kwa njia ya Roho wake. Maana Roho huchunguza kila kitu hata mambo ya ndani kabisa ya Mungu.
- 11 Nani awezaye kujua mambo ya ndani ya mtu isipokuwa roho yake mtu huyo? Hali kadhalika, hakuna ajuaye mambo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu.
- 12 Sasa sisi hatukuipokea roho ya ulimwengu, bali tumepokea Roho atokaye kwa Mungu ili atuwezeshe kujua yale tuliyojaliwa na Mungu.
- 13 Basi sisi twafundisha, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya binadamu, bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho.
- 14 Mtu wa kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu mtupu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho.
- 15 Lakini mtu aliye na huyo Roho anaweza kubainisha ubora wa kila kitu, naye mwenyewe hahukumiwi na mtu mwingine.
- 16 Maandiko yasema: "Nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Nani awezaye kumshauri?" Lakini sisi tunayo akili ya Kristo.