고린도전서 7장 Swahili NT
- 1 Yahusu sasa mambo yale mliyoandika: naam, ni vizuri kama mtu haoi;
- 2 lakini kwa sababu ya hatari ya uzinzi, basi, kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe.
- 3 Mume atimize wajibu alio nao kwa mkewe, naye mke atimize wajibu alio nao kwa mumewe.
- 4 Mke hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mumewe anayo; hali kadhalika naye mume, hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mkewe anayo.
- 5 Msinyimane haki zenu, isipokuwa kama mnaafikiana kufanya hivyo kwa kitambo tu, ili mpate nafasi nzuri ya kusali. Kisha rudianeni tena mara, ili Shetani asije akawajaribu kwa sababu ya udhaifu wenu.
- 6 Ninayowaambieni sasa ni mawaidha, si amri.
- 7 Ningependa watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mmoja anacho kipaji chake kutoka kwa Mungu; mmoja kipaji hiki na mwingine kile.
- 8 Basi, wale ambao hawajaoana na wale walio wajane nawaambia kwamba ni vema kuendelea kuwa kama mimi nilivyo.
- 9 Hata hivyo, kama mtu hawezi kujizuia basi, na aoe; maana ni afadhali zaidi kuoa kuliko kuwaka tamaa.
- 10 Kwa wale waliooa ninayo amri, tena si yangu, ila ni ya Bwana: mke asiachane na mumewe;
- 11 lakini kama akiachana naye, basi abaki bila kuolewa; ama la, apatanishwe na mume wake. Mume naye asimpe talaka mkewe.
- 12 Kwa wale wengine, (mimi binafsi, si Bwana) nasema hivi: Ikiwa mwanamume Mkristo anaye mke asiyeamini, na huyo mwanamke akakubali kuendelea kuishi naye, asimpe talaka.
- 13 Na, kama mwanamke Mkristo anaye mume asiyeamini, na huyo mwanamume akakubali kuendelea kuishi naye, basi, asimpe talaka mumewe.
- 14 Kwa maana huyo mume asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mkewe; na huyo mke asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mumewe. Vinginevyo watoto wao wangekuwa si wa Mungu; kumbe sasa ni watoto wake Mungu.
- 15 Hata hivyo, ikiwa yule asiyeamini anataka kumwacha mwenzake aliye Mkristo, basi, na amwache tu. Hapo huyo Mkristo, mume au mke, atakuwa huru. Maana Mungu amewaiteni ninyi muishi kwa amani.
- 16 Wewe mama Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mume wako? Au wewe mume Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mkeo?
- 17 Kwa vyovyote kila mmoja na aishi kufuatana na vipaji alivyogawiwa na Bwana, na kama alivyoitwa na Mungu. Hili ndilo agizo langu kwa makanisa yote.
- 18 Kama mtu aliitwa akiwa ametahiriwa, basi asijisingizie kwamba hakutahiriwa; na kama alipoitwa hakuwa ametahiriwa, basi na asitahiriwe.
- 19 Maana kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; kilicho muhimu ni kuzishika amri za Mungu.
- 20 Basi, kila mmoja na abaki kama alivyokuwa wakati alipoitwa.
- 21 Je, wewe ulikuwa mtumwa wakati ulipoitwa? Sawa, usijali; lakini ukipata fursa ya kuwa huru, itumie.
- 22 Maana yeye aliyeitwa na Bwana akiwa mtumwa huyo huwa mtu huru wa Bwana. Hali kadhalika naye aliyeitwa akiwa mtu huru, huwa mtumwa wa Kristo.
- 23 Nyote mmenunuliwa kwa bei; kwa hiyo msiwe tena watumwa wa watu.
- 24 Ndugu zangu, kila mmoja wenu basi, na abaki na Mungu kama alivyokuwa wakati alipoitwa.
- 25 Sasa, kuhusu mabikira na waseja, sina amri kutoka kwa Bwana; lakini natoa maoni yangu mimi ambaye kwa huruma yake Bwana nastahili kuaminiwa.
- 26 Basi, kutokana na shida iliyopo sasa nadhani ingefaa mtu abaki kama alivyo.
- 27 Je, umeoa? Basi, usitake kuachana na mkeo. Wewe hukuoa? Basi, usitake kuoa.
- 28 Lakini ikiwa utaoa hutakuwa umetenda dhambi; na msichana akiolewa hatakuwa ametenda dhambi. Hao watakaooana watapatwa na matatizo ya dunia hii, lakini mimi ningependa hayo yasiwapate ninyi.
- 29 Ndugu, nataka kusema hivi: muda uliobaki ni mfupi. Na tangu sasa wale waliooa na waishi kama vile hawakuoa;
- 30 wenye kulia wawe kama hawalii, na wenye kufurahi wawe kama hawafurahi; wanaonunua wawe kama hawana kitu;
- 31 nao wenye shughuli na dunia hii wawe kama vile hawana shughuli sana nayo. Maana ulimwengu huu, kama tuujuavyo, unapita.
- 32 Ningependa ninyi msiwe na wasiwasi. Mtu asiye na mke hujishughulisha na kazi ya Bwana jinsi atakavyompendeza Bwana.
- 33 Mtu aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia jinsi atakavyompendeza mkewe,
- 34 naye amegawanyika. Mwanamke asiyeolewa au bikira hujishughulisha na mambo ya Bwana apate kujitolea mwili na roho kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii jinsi atakavyompendeza mumewe.
- 35 Nawaambieni haya kwa faida yenu, na si kwa kuwawekeeni kizuio. Nataka tu muwe na mpango unaofaa, mpate kumtumikia Bwana kwa moyo na nia moja.
- 36 Kama mtu anaona kwamba hamtendei vyema mchumba wake asipomwoa, na kama tamaa zake zinamshinda, na afanye atakavyo; waoane tu; hatakuwa ametenda dhambi.
- 37 Lakini kama huyo mwanamume akiamua kwa hiari moyoni mwake kutooa na kama anaweza kuzitawala tamaa zake na kuamua namna ya kufanya, basi, anafanya vizuri zaidi asipomwoa huyo mwenzake bikira.
- 38 Kwa maneno mengine: yule anayeamua kumwoa huyo mchumba wake anafanya vema; naye anayeamua kutomwoa anafanya vema zaidi.
- 39 Mwanamke huwa amefungwa na mumewe kwa muda wote mumewe aishipo. Lakini mumewe akifa, mama huyo yuko huru, na akipenda anaweza kuolewa na mtu yeyote, mradi tu iwe Kikristo.
- 40 Lakini, nionavyo mimi, atakuwa na heri zaidi kama akibaki hivyo alivyo. Hayo ni maoni yangu, na nafikiri mimi pia ninaye Roho wa Mungu.