고린도후서 2장 Swahili NT
- 1 Basi nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni.
- 2 Maana nikiwahuzunisha ninyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha!
- 3 Ndiyo maana niliwaandikia--sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na ninyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba, mimi nikifurahi, ninyi nyote pia mnafurahi.
- 4 Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha ninyi, bali kwa ajili ya kuwaonyesheni kwamba nawapenda mno.
- 5 Ikiwa kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi--ila amewahuzunisha ninyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi.
- 6 Adhabu aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha.
- 7 Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa.
- 8 Kwa hiyo nawasihi: mwonyesheni kwamba mnampenda.
- 9 Madhumuni yangu kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo.
- 10 Mkimsamehe mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe--kama kweli ninacho cha kusamehe--nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu,
- 11 ili tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo.
- 12 Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa ajili ya kazi ya Bwana.
- 13 Lakini nilifadhaika sana kwa kutomkuta ndugu yetu Tito. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda Makedonia.
- 14 Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali.
- 15 Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote wanaookolewa na wanaopotea.
- 16 Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo?
- 17 Sisi si kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo.