고린도후서 6장 Swahili NT
- 1 Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure.
- 2 Mungu asema hivi: "Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia." Basi, sasa ndio wakati wa kufaa, sasa ndiyo siku ya wokovu!
- 3 Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuio chochote.
- 4 Badala yake, tunajionyesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu.
- 5 Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula.
- 6 Tunajionyesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki,
- 7 kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu upande wa kulia na upande wa kushoto.
- 8 Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli;
- 9 kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote, kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni wazima kabisa.
- 10 Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini hohehahe, lakini twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu.
- 11 Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa.
- 12 Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu ninyi wenyewe, na si kwa upande wetu.
- 13 Sasa nasema nanyi kama watoto wangu, wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya.
- 14 Msiambatane na watu wasioamini. Je, wema na uovu vyapatana kweli? Mwanga na giza vyawezaje kukaa pamoja?
- 15 Kristo anawezaje kupatana na Shetani? Muumini ana uhusiano gani na asiyeamini?
- 16 Hekalu la Mungu lina uhusiano gani na sanamu za uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu mwenyewe alivyosema: "Nitafanya makao yangu kwao, na kuishi kati yao; Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu."
- 17 Kwa hiyo Bwana asema pia: "Ondokeni kati yao, mkajitenge nao, msiguse kitu najisi, nami nitawapokea.
- 18 Mimi nitakuwa Baba yenu, nanyi mtakuwa watoto wangu, waume kwa wake, asema Bwana Mwenye Uwezo."