갈라디아서 4장 Swahili NT
- 1 Basi, nasema hivi: mrithi, akiwa bado mtoto, hawi tofauti na mtumwa ingawaje mali yote ni yake.
- 2 Wakati huo wote yuko chini ya walezi na wadhamini mpaka wakati ule uliowekwa na baba yake.
- 3 Hali kadhalika na sisi tulipokuwa bado watoto, tulikuwa watumwa wa pepo watawala wa ulimwengu.
- 4 Lakini wakati ule maalumu ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanawe aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini ya Sheria
- 5 apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya Sheria ili sisi tufanywe wana wa Mungu.
- 6 Kwa vile sasa ninyi ni wana, Mungu amemtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwenu, Roho ambaye hulia "Aba," yaani "Baba."
- 7 Basi, wewe si mtumwa tena, bali mwana. Na ikiwa ni mwana, basi, wewe utapokea yote Mungu aliyowawekea watoto wake.
- 8 Zamani hamkumjua Mungu na hivyo mkatumikia miungu isiyo miungu kweli.
- 9 Lakini sasa, kwa vile mnamjua Mungu, au tuseme mnajulikana na Mungu, mnawezaje tena kurudi kwa wale pepo maskini na dhaifu hata kutaka kuwatumikia tena?
- 10 Bado mnaadhimisha siku, miezi na miaka!
- 11 Nahofu kwamba labda kazi niliyoifanya kwa ajili yenu imepotea bure!
- 12 Ndugu, nawasihi muwe kama mimi, kwa vile hata mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea ubaya wowote.
- 13 Mnajua kwamba ugonjwa wangu ndio ulionipatia fursa ya kuwahubirieni Habari Njema kwa mara ya kwanza.
- 14 Hata hivyo, wakati ule hamkunidharau wala kunikataa kwa sababu ya udhaifu wangu ingawa mlishawishiwa kufanya hivyo; lakini mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama vile ningekuwa Kristo Yesu mwenyewe.
- 15 Mlikuwa wenye furaha; sasa kumetokea nini? Naapa kwamba wakati ule mngaliweza hata kuyang'oa macho yenu na kunipa mimi.
- 16 Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa sababu ya kuwaambieni ukweli?
- 17 Hao watu wengine wanawahangaikia ninyi, lakini nia zao si njema. Wanataka kuwatenganisha nami ili ninyi muwahangaikie wao.
- 18 Kwa kweli ni jambo jema daima kuwahangaikia wengine katika mambo mema, na si tu wakati mimi nipo pamoja nanyi.
- 19 Watoto wangu, kama vile mama mja mzito anavyotaabika wakati wa kujifungua, mimi nataabika tena kwa ajili yenu mpaka hapo hali yake Kristo itakapoundwa ndani yenu.
- 20 Laiti ningekuwa pamoja nanyi sasa, maana ningalipata msimamo ufaao juu yenu! Nina wasiwasi sana nanyi!
- 21 Niambieni, enyi mnaopenda kutawaliwa na sheria: Je, mnasikia isemavyo Sheria?
- 22 Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Abrahamu alikuwa na watoto wawili: mmoja kwa mwanamke mtumwa, na wa pili kwa mwanamke huru.
- 23 Yule wa mwanamke mtumwa alizaliwa kama kawaida, lakini yule wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu.
- 24 Mambo hayo yamekuwa mfano; mama hao wawili ni mfano wa maagano mawili; la kwanza ni lile lililofanyika mlimani Sinai, mwakilishi wake ni Hagari, na watoto wake wanazaliwa utumwani.
- 25 Hagari anawakilisha mlima Sinai ulioko Arabia, na ni mfano wa Yerusalemu ya sasa, ulio mtumwa pamoja na watoto wake.
- 26 Lakini Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu.
- 27 Maana imeandikwa: "Furahi, ewe uliye tasa usiyezaa; paaza sauti wewe usiyepata kujifungua mtoto; maana watoto wa yule aliyeachwa ni wengi zaidi kuliko wa yule aliye na mume."
- 28 Sasa, basi, ndugu zangu, ninyi ni watoto wa Mungu kutokana na ahadi yake kama alivyokuwa Isaka.
- 29 Lakini kama vile siku zile yule mtoto aliyezaliwa kwa njia ya kawaida alimdhulumu yule aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho wa Mungu, vivyo hivyo na siku hizi.
- 30 Lakini Maandiko Matakatifu yasemaje? Yasema: "Mfukuze mama mtumwa pamoja na mwanawe; maana mtoto wa mtumwa hatarithi pamoja na mtoto wa mama huru."
- 31 Kwa hiyo, basi, ndugu, sisi si watoto wa mtumwa bali wa mama huru.