에베소서 1장 Swahili NT
- 1 Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, nawaandikia ninyi watu wa Mungu huko Efeso, mlio waaminifu katika kuungana na Kristo Yesu.
- 2 Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
- 3 Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni.
- 4 Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake,
- 5 Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia.
- 6 Basi, tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu katika Mwanae mpenzi!
- 7 Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake
- 8 aliotukirimia bila kipimo! Kwa hekima na ujuzi wake wote
- 9 Mungu alitekeleza kile alichonuia, akatujulisha mpango wake uliofichika, ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza kwa njia ya Kristo.
- 10 Mpango huo ambao angeutimiza wakati utimiapo ni kukusanya pamoja viumbe vyote, kila kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo.
- 11 Kila kitu hufanywa kufuatana na mpango na uamuzi wa Mungu; naye Mungu ametuteua sisi tuwe watu wake kwa mapenzi yake katika kuungana na Kristo, kufuatana na azimio alilofanya tangu mwanzo.
- 12 Basi, sisi tuliotangulia kumtumainia Kristo tunapaswa kuusifu utukufu wa Mungu!
- 13 Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonyesha kuwa ninyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia.
- 14 Huyu Roho ni dhamana ya kurithi yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu utukufu wake!
- 15 Kwa sababu hiyo, tangu niliposikia juu ya imani yenu kwa Bwana Yesu na mapendo yenu kwa watu wa Mungu,
- 16 sijaacha kamwe kumshukuru Mungu kwa ajili yenu. Ninawakumbuka katika sala zangu
- 17 ili Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo Baba mtukufu, awajalieni Roho wake atakayewapa hekima na kuwafunulieni Mungu mpate kumjua.
- 18 Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake,
- 19 mpate kutambua jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Uwezo huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na nguvu ile kuu mno
- 20 aliyomfufua nayo Kristo kutoka wafu, akamketisha kulia kwake mbinguni.
- 21 Huko, Kristo anatawala juu ya kila tawala, mamlaka, enzi na ukuu; anatawala juu ya kila cheo kiwezacho kutajwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ujao.
- 22 Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa kanisa akiwa mkuu wa vitu vyote.
- 23 Kanisa ni mwili wa Kristo, na ukamilifu wake yeye anayekamilisha vitu vyote kila mahali.