에베소서 3장 Swahili NT
- 1 Kutokana na hayo, mimi Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu, namwomba Mungu.
- 2 Bila shaka mmekwisha sikia kwamba Mungu, kwa neema yake, alinikabidhi kazi hii niifanye kwa faida yenu.
- 3 Mimi nilijulishwa kwa njia ya ufunuo mpango wake uliofichika. (Nimeandika kwa ufupi juu ya jambo hili,
- 4 nanyi mkiyasoma maneno yangu mtaweza kujua jinsi ninavyoielewa siri hiyo ya Kristo.)
- 5 Zamani watu hawakujulishwa siri hiyo; lakini sasa Mungu amewajulisha mitume na manabii wake watakatifu kwa njia ya Roho.
- 6 Siri yenyewe ni hii: kwa njia ya Habari Njema watu wa mataifa mengine wanapata sehemu yao pamoja na Wayahudi katika zile baraka za Mungu; wao ni viungo vya mwili uleule, na wanashiriki ahadi ileile aliyofanya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.
- 7 Mimi nimefanywa kuwa mtumishi wa Habari Njema kwa neema ya pekee aliyonijalia Mungu kwa uwezo wake mkuu.
- 8 Mimi ni mdogo kuliko watu wote wa Mungu; lakini amenijalia neema yake, ili niwahubirie watu wa mataifa utajiri wake Kristo usiopimika,
- 9 tena niwaangazie watu wote waone jinsi mpango wa Mungu uliofichika unavyotekelezwa. Mungu aliye Muumba wa vitu vyote alificha siri hiyo yake tangu milele,
- 10 kusudi, sasa kwa njia ya kanisa, wakuu na wenye enzi wa mbinguni wapate kuitambua hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi.
- 11 Mungu alifanya jambo hilo kufuatana na azimio lake la milele ambalo amelifanya kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
- 12 Basi, katika kuungana na Kristo, na kwa njia ya imani katika Kristo, sisi tunathubutu kumkaribia Mungu kwa uhodari.
- 13 Kwa hiyo, nawaombeni msife moyo kwa sababu ya mateso ninayopata kwa ajili yenu, maana hayo ni kwa ajili ya utukufu wenu.
- 14 Kwa sababu hiyo, nampigia magoti Baba,
- 15 aliye asili ya jamaa zote duniani na mbinguni.
- 16 Namwomba Mungu, kadiri ya utajiri wa utukufu wake, awajalieni kwa uwezo wa Roho wake, nguvu ya kuwa imara ndani yenu,
- 17 naye Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani. Namwomba mpate kuwa na mzizi na msingi katika mapendo
- 18 kusudi muweze kufahamu pamoja na watu wote wa Mungu jinsi upendo wa Kristo ueneavyo kwa mapana na marefu, kwa kimo na kina.
- 19 Naam, mpate kujua upendo wa Kristo upitao elimu yote, mjazwe kabisa utimilifu wote wa Mungu.
- 20 Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu, aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria;
- 21 kwake Mungu uwe utukufu katika kanisa na katika Kristo Yesu, nyakati zote, milele na milele! Amina.