에베소서 6장 Swahili NT
- 1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu Kikristo maana hili ni jambo jema.
- 2 "Waheshimu Baba na mama yako," hii ndiyo amri ya kwanza ambayo imeongezewa ahadi, yaani,
- 3 "Upate fanaka na miaka mingi duniani."
- 4 Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo.
- 5 Enyi watumwa, watiini mabwana zenu hapa duniani kwa hofu na tetemeko; fanyeni hivyo kwa unyofu wa moyo kana kwamba mnamtumikia Kristo.
- 6 Fanyeni hivyo si tu wakati wanapowatazama ili mjipendekeze kwao, bali tumikieni kwa moyo kama atakavyo Mungu kwa sababu ninyi ni watumishi wa Kristo.
- 7 Muwe radhi kutumikia kwa ajili ya Bwana na si kwa ajili ya watu.
- 8 Kumbukeni kwamba kila mtu mwenye kutenda mema, awe mtumwa au mtu huru, atapokea tuzo lake kutoka kwa Bwana.
- 9 Nanyi mnaotumikiwa, watendeeni vivyo hivyo watumwa wenu, na acheni kutumia vitisho. Kumbukeni kwamba ninyi pia kama vile wao, mnaye Bwana yuleyule mbinguni, kwake cheo cha mtu si kitu.
- 10 Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu.
- 11 Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu mbaya za Ibilisi.
- 12 Maana vita vyenu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu wanaomiliki ulimwengu huu wa giza.
- 13 Kwa sababu hiyo, vaeni silaha za Mungu ili siku ile itakapofika muweze kuyapinga mashambulio ya adui; na mkisha pigana mpaka mwisho, muwe bado thabiti.
- 14 Basi, simameni imara! Ukweli uwe kama ukanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama vazi la kujikinga kifuani,
- 15 na hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani iwe kama viatu miguuni mwenu.
- 16 Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu.
- 17 Upokeeni wokovu kama kofia yenu ya chuma, na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu.
- 18 Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu.
- 19 Niombeeni nami pia ili niongeapo Mungu anijalie cha kusema, niweze kuwajulisha watu fumbo la Habari Njema kwa uthabiti.
- 20 Mimi ni balozi kwa ajili ya Habari Njema hiyo ingawa sasa niko kifungoni. Ombeni, basi, ili niweze kuwa hodari katika kuitangaza kama inipasavyo.
- 21 Tukiko, ndugu yetu mpenzi na mtumishi mwaminifu wa Bwana, atawapeni habari zangu zote mpate kujua ninachofanya.
- 22 Namtuma kwenu awapeni habari zetu mpate kuwa na moyo.
- 23 Ninawatakieni ninyi ndugu amani, upendo na imani kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.
- 24 Nawatakia neema ya Mungu wote wanaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa mapendo yasiyo na mwisho.