골로새서 4장 Swahili NT
- 1 Nanyi wakuu, watendeeni watumwa wenu kwa uadilifu na haki, mkikumbuka kwamba nanyi pia mnaye Bwana mbinguni.
- 2 Dumuni katika sala, na mnaposali muwe waangalifu, mkimshukuru Mungu.
- 3 Vilevile, mtuombee sisi pia ili Mungu atupe fursa ya kuuhubiri ujumbe wake kuhusu siri ya Kristo. Kwa ajili hiyo mimi niko sasa kifungoni.
- 4 Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa namna itakayodhihirisha siri hiyo.
- 5 Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini, mkitumia vizuri kila nafasi mliyo nayo.
- 6 Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na ya kuvutia, na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja.
- 7 Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote.
- 8 Ndiyo maana namtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa kuwaambieni habari zetu.
- 9 Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote yanayofanyika hapa.
- 10 Aristarko, ambaye yuko kifungoni pamoja nami, anawasalimuni; hali kadhalika Marko, binamu yake Barnaba, (mmekwisha pata maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni).
- 11 Naye Yoshua aitwaye Yusto, anawasalimuni. Miongoni mwa Wayahudi waliokwisha pokea imani, hawa tu peke yao, ndio wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya Utawala wa Mungu; nao wamekuwa msaada mkubwa kwangu.
- 12 Epafra, mwananchi mwenzenu na mtumishi wa Kristo Yesu anawasalimuni. Daima anawaombeeni ninyi kwa bidii ili mpate kusimama imara, mkomae na kuwa thabiti kabisa katika mambo yote anayotaka Mungu.
- 13 Naweza kushuhudia kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu na kwa ajili ya watu wa Laodikea na Hierapoli.
- 14 Luka, daktari wetu mpenzi, na Dema, wanawasalimuni.
- 15 Salamu zetu kwa ndugu zetu wa Laodikea; msalimuni dada Nimfa pamoja na jumuiya yote ya waumini inayokutana nyumbani kwake.
- 16 Mkisha soma barua hii, hakikisheni kwamba inasomwa na Wakristo wa Laodikea; na ninyi fanyeni mpango mpate kuisoma barua waliyoipata kwao.
- 17 Mwambieni Arkipo aitekeleze vizuri ile huduma aliyokabidhiwa na Bwana.
- 18 Naandika haya kwa mkono wangu mwenyewe: Salamu kutoka kwangu, mimi Paulo. Kumbukeni kwamba niko kifungoni. Neema ya Mungu iwe nanyi.