데살로니가전서 5장 Swahili NT
- 1 Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira yatakapotukia mambo haya.
- 2 Maana ninyi wenyewe mwajua kwamba Siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku.
- 3 Watu watakapokuwa wanasema: "Kila kitu ni shwari na salama" ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo.
- 4 Lakini ninyi ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi.
- 5 Ninyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza.
- 6 Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi.
- 7 Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku.
- 8 Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma.
- 9 Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,
- 10 ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa.
- 11 Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana ninyi kwa ninyi kama mnavyofanya sasa.
- 12 Ndugu, tunawaombeni muwastahi wale wanaofanya kazi kati yenu, wale wanaowaongoza na kuwafundisheni kuhusu maisha ya Kikristo.
- 13 Wapeni heshima kubwa na kuwapenda kwa sababu ya kazi wanayofanya. Muwe na amani kati yenu.
- 14 Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote.
- 15 Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote.
- 16 Furahini daima,
- 17 salini kila wakati
- 18 na muwe na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu.
- 19 Msimpinge Roho Mtakatifu;
- 20 msidharau unabii.
- 21 Pimeni kila kitu: zingatieni kilicho chema,
- 22 na epukeni kila aina ya uovu.
- 23 Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu--roho, mioyo na miili yenu--mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
- 24 Yeye anayewaita ninyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu.
- 25 Ndugu, tuombeeni na sisi pia.
- 26 Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo.
- 27 Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii.
- 28 Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.