데살로니가후서 3장 Swahili NT
- 1 Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili ujumbe wa Bwana uzidi kuenea upesi na kupokelewa kwa heshima kama vile ulivyo kati yenu.
- 2 Ombeni pia ili Mungu atuokoe na watu wapotovu na waovu, maana si wote wanaoamini ujumbe huu.
- 3 Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu.
- 4 Naye Bwana anatupatia tumaini kubwa juu yenu, na hatuna shaka kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaambieni.
- 5 Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika uvumilivu tunaopewa na Kristo.
- 6 Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa.
- 7 Ninyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu;
- 8 hatukula chakula kwa mtu yeyote bila ya kumlipa. Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu.
- 9 Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano.
- 10 Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, "Mtu asiyefanya kazi, asile."
- 11 Tunasema mambo hayo kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine.
- 12 Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru na kuwaonya watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe.
- 13 Lakini ninyi ndugu, msichoke kutenda mema.
- 14 Huenda kwamba huko kuna mtu ambaye hatautii huu ujumbe tunaowapelekeeni katika barua hii. Ikiwa hivyo, basi, mfichueni mtu huyo na msiwe na uhusiano wowote naye kusudi aone aibu.
- 15 Lakini msimtendee mtu huyo kama adui, bali mwonyeni kama ndugu.
- 16 Bwana mwenyewe ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote.
- 17 Kwa mkono wangu mwenyewe naandika hivi: Salamu kutoka kwa Paulo! Hivi ndivyo ninavyotia sahihi kila barua; ndivyo ninavyoandika.
- 18 Tunawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.