디모데전서 2장 Swahili NT
- 1 Kwanza kabisa, basi naomba dua, sala, maombi na sala za shukrani zitolewe kwa Mungu kwa ajili ya watu wote,
- 2 kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema.
- 3 Jambo hili ni jema na lampendeza Mungu Mwokozi wetu,
- 4 ambaye anataka watu wote waokolewe na wapate kuujua ukweli.
- 5 Maana yuko Mungu mmoja, na pia yuko mmoja anayewapatanisha watu na Mungu, binadamu Kristo Yesu,
- 6 ambaye alijitoa mwenyewe kuwakomboa watu wote. Huo ulikuwa uthibitisho, wakati ufaao ulipowadia.
- 7 Kwa sababu hiyo mimi nilitumwa niwe mtume na mwalimu wa watu wa mataifa, niutangaze ujumbe wa imani na ukweli. Nasema ukweli; sisemi uongo!
- 8 Basi, popote mnapokutana kufanya ibada nataka wanaume wasali, watu waliojitolea kweli na ambao wanaweza kuinua mikono yao wakisali bila hasira wala ubishi.
- 9 Hali kadhalika, nawataka wanawake wawe wanyofu na wenye busara kuhusu mavazi yao; wavae sawasawa na si kwa urembo wa mitindo ya kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa,
- 10 bali kwa matendo mema kama iwapasavyo wanawake wamchao Mungu.
- 11 Wanawake wanapaswa kukaa kimya na kuwa wanyenyekevu wakati wa kujifunza.
- 12 Mimi simruhusu mwanamke amfundishe au amtawale mwanamume; anapaswa kukaa kimya.
- 13 Maana Adamu aliumbwa kwanza, halafu Hawa.
- 14 Na wala si Adamu aliyedanganywa; bali mwanamke ndiye aliyedanganywa, akaivunja sheria ya Mungu.
- 15 Hata hivyo, mwanamke ataokolewa kwa kupata watoto, kama akidumu katika imani, upendo, utakatifu na unyofu.