디모데후서 3장 Swahili NT
- 1 Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu.
- 2 watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu;
- 3 watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema;
- 4 watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu.
- 5 Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo.
- 6 Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za kila aina;
- 7 wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi kuufikia ujuzi wa huo ukweli.
- 8 Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre walivyompinga Mose.
- 9 Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre.
- 10 Wewe lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, subira yangu,
- 11 udhalimu na mateso yangu. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra. Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote.
- 12 Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe.
- 13 Watu waovu na wadanyanyifu watazidi kuwa waovu zaidi na zaidi kwa kuwadanganya wengine na kudanganyika wao wenyewe.
- 14 Lakini wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa, ukaukubali kabisa. Unawajua wale waliokuwa walimu wako.
- 15 Unakumbuka kwamba tangu utoto wako umeyajua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu.
- 16 Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili,
- 17 ili mtu anayemtumikia Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila tendo jema.