디도서 2장 Swahili NT
- 1 Lakini wewe unapaswa kuhubiri mafundisho safi.
- 2 Waambie wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu.
- 3 Hali kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe wachongezi, au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema,
- 4 ili wawazoeze kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto,
- 5 wawe na kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa.
- 6 Kadhalika, wahimize vijana wawe na kiasi.
- 7 Katika mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe na uzito katika mafundisho yako.
- 8 Maneno yako yasiwe na hitilafu yoyote ili adui zako waaibike wasipopata chochote kibaya cha kusema juu yetu.
- 9 Watumwa wanapaswa kuwatii wakuu wao na kuwapendeza katika mambo yote. Wasibishane nao,
- 10 au kuiba vitu vyao. Badala yake wanapaswa kuonyesha kwamba wao ni wema na waaminifu daima, ili, kwa matendo yao yote, wayapatie sifa njema mafundisho juu ya Mungu, Mwokozi wetu.
- 11 Maana neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote.
- 12 Neema hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi maisha adili na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa,
- 13 tukiwa tunangojea siku ile ya heri tunayoitumainia, wakati utakapotokea utukufu wa Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
- 14 Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda mema.
- 15 Basi, fundisha mambo hayo na tumia mamlaka yako yote ukiwahimiza na kuwaonya wasikilizaji wako. Mtu yeyote na asikudharau.