빌레몬서 1장 Swahili NT
- 1 Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu
- 2 na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkupo.
- 3 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana yesu Kristo.
- 4 Kila wakati ninaposali nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu
- 5 maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana wetu Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu.
- 6 Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo.
- 7 Ndugu, upendo wako yameniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu.
- 8 Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya.
- 9 Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake.
- 10 Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni.
- 11 Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia.
- 12 Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe.
- 13 Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Habari Njema.
- 14 Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika.
- 15 Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima.
- 16 Na sasa yeye si mtumwa tu, ila ni bora zaidi ya mtumwa: yeye ni ndugu yetu mpenzi. Na wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana.
- 17 Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe.
- 18 Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi.
- 19 Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: Mimi Paulo nitalipa! (Tena sina haja ya kusema kwamba wewe unalo deni kwangu la nafsi yako.)
- 20 Haya, basi, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo.
- 21 Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba.
- 22 Pamoja na hayo, nitayarishie chumba kwani natumaini kwamba kwa sala zenu, Mungu atanijalia niwatembeleeni.
- 23 Epafra, mfungwa mwenzangu kwa ajili ya Kristo Yesu, anakusalimu.
- 24 Nao akina Marko, Aristarko, Dema na Luka, wafanyakazi wenzangu, wanakusalimu.
- 25 Nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.