히브리서 10장 Swahili NT
- 1 Sheria ya Wayahudi si picha kamili ya mambo yale halisi: ni kivuli tu cha mema yanayokuja. Dhabihu zilezile hutolewa daima, mwaka baada ya mwaka. Sheria yawezaje, basi, kwa njia ya dhabihu hizo, kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu?
- 2 Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na dhabihu hizo zote zingekoma.
- 3 Lakini dhabihu hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao.
- 4 Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi.
- 5 Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: "Hukutaka dhabihu wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili.
- 6 Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi.
- 7 Hapo nikasema: Niko hapa ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha Sheria."
- 8 Kwanza alisema: "Hutaki, wala hupendezwi na dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi." Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na Sheria.
- 9 Kisha akasema: "Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako." Hivyo Mungu alibatilisha dhabihu za zamani na mahali pake akaweka dhabihu nyingine moja.
- 10 Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza mapenzi ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile dhabihu ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha.
- 11 Kila kuhani Myahudi humhudumia Mungu kila siku, akitoa dhabibu zilezile mara nyingi, dhabibu ambazo haziwezi kuondoa dhambi.
- 12 Lakini Kristo alitoa dhabihu moja tu kwa ajili ya dhambi, dhabihu ifaayo milele, kisha akaketi upande wa kulia wa Mungu.
- 13 Huko anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake.
- 14 Basi, kwa dhabihu yake moja tu, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa dhambi zao.
- 15 Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema:
- 16 "Hili ndilo agano nitakalofanya nao, katika siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao."
- 17 Kisha akaongeza kusema: "Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu."
- 18 Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa dhabihu za kuondoa dhambi.
- 19 Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu.
- 20 Yeye ametufungulia njia mpya na yenye uzima kupitia lile pazia, yaani kwa njia ya mwili wake mwenyewe.
- 21 Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu.
- 22 Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi.
- 23 Tushikilie imara tumaini lile tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
- 24 Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema.
- 25 Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, Siku ile ya Bwana inakaribia.
- 26 Maana, tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kufahamu ukweli, hakuna dhabihu iwezayo kutolewa tena kwa ajili ya kuondoa dhambi.
- 27 Linalobaki ni kungojea tu kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza wote wanaompinga.
- 28 Mtu yeyote asiyeitii Sheria ya Mose, huuawa bila ya huruma kukiwa na ushahidi wa watu wawili au watatu.
- 29 Je, mtu yule anayempuuza Mwana wa Mungu na kuidharau damu ya agano la Mungu iliyomtakasa, mtu anayemtukana Roho wa Mungu, anastahili kupata adhabu kali ya namna gani?
- 30 Maana tunamfahamu yule aliyesema, "Mimi nitalipiza kisasi, mimi nitalipiza," na ambaye alisema pia, "Bwana atawahukumu watu wake."
- 31 Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha mno!
- 32 Kumbukeni yaliyotokea siku zile za kwanza mlipoangaziwa mwanga wa Mungu. Ingawa siku zile mlipatwa na mateso mengi, ninyi mlistahimili.
- 33 Mara nyingine mlitukanwa na kufedheheshwa hadharani; mara nyingine mlikuwa radhi kuungana na wale walioteswa namna hiyohiyo.
- 34 Mlishiriki mateso ya wafungwa, na mliponyang'anywa mali yenu mlistahimili kwa furaha, maana mlijua kwamba mnayo mali bora zaidi na ya kudumu milele.
- 35 Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatieni tuzo kubwa.
- 36 Mnahitaji kuwa na uvumilivu, ili mweze kufanya anayotaka Mungu na kupokea kile alichoahidi.
- 37 Maana kama yasemavyo Maandiko: "Bado kidogo tu, na yule anayekuja, atakuja, wala hatakawia.
- 38 Lakini mtu wangu aliye mwadilifu ataamini na kuishi; walakini akirudi nyuma, mimi sitapendezwa naye."
- 39 Basi, sisi hatumo miongoni mwa wale wanaorudi nyuma na kupotea, ila sisi tunaamini na tunaokolewa.