히브리서 3장 Swahili NT
- 1 Ndugu zangu watu wa Mungu ambao mmeitwa na Mungu, fikirini juu ya Yesu ambaye Mungu alimtuma awe Kuhani Mkuu wa imani tunayoiungama.
- 2 Yeye alikuwa mwaminifu kwa Mungu aliyemteua kufanya kazi yake kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.
- 3 Mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe. Hali kadhalika naye Yesu anastahili heshima kubwa zaidi kuliko Mose.
- 4 Kila nyumba hujengwa na mjenzi fulani--na Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote.
- 5 Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye.
- 6 Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi ni nyumba yake kama tukizingatia uhodari wetu na uthabiti wetu katika kile tunachotumainia.
- 7 Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo,
- 8 msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu; kama walivyokuwa siku ile kule jangwani,
- 9 Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza, asema Bwana, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu kwa miaka arobaini.
- 10 Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema, Fikira za watu hawa zimepotoka, hawajapata kamwe kuzijua njia zangu.
- 11 Basi, nilikasirika, nikaapa: Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."
- 12 Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai.
- 13 Maadamu hiyo "Leo" inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi.
- 14 Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni.
- 15 Maandiko yasema hivi: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu."
- 16 Ni akina nani basi, waliosikia sauti ya Mungu wakamwasi? Ni wale wote walioongozwa na Mose kutoka Misri.
- 17 Mungu aliwakasirikia akina nani kwa miaka arobaini? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi, maiti zao zikatapakaa kule jangwani.
- 18 Mungu alipoapa: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko," alikuwa anawasema akina nani? Alikuwa anasema juu ya hao walioasi.
- 19 Basi, twaona kwamba hawakuingia huko kwa sababu hawakuamini.