야고보서 1장 Swahili NT
- 1 Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia ninyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salaam!
- 2 Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali,
- 3 kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu.
- 4 Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.
- 5 Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.
- 6 Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo.
- 7 Mtu wa namna hiyo, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote,
- 8 asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.
- 9 Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza,
- 10 naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini.
- 11 Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake.
- 12 Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili atapewa tuzo la uzima ambalo Mungu aliwaahidia wale wanaompenda.
- 13 Kama mtu akijaribiwa, asiseme: "Ninajaribiwa na Mungu." Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote.
- 14 Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya.
- 15 Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo.
- 16 Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike!
- 17 Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu.
- 18 Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe namna ya matunda ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.
- 19 Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini asiwe mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika.
- 20 Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki.
- 21 Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea ule ujumbe uliopandwa mioyoni mwenu, ambao waweza kuziokoa nafsi zenu.
- 22 Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo.
- 23 Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo.
- 24 Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo.
- 25 Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya.
- 26 Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe.
- 27 Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.