야고보서 4장 Swahili NT
- 1 Mapigano na magombano yote kati yenu yanatoka wapi? Hutoka katika tamaa zenu mbaya ambazo hupigana daima ndani yenu.
- 2 Mnatamani vitu na kwa vile hamvipati mko tayari kuua; mwatamani sana kupata vitu, lakini hamvipati, hivyo mnagombana na kupigana. Hampati kile mnachotaka kwa sababu hamkiombi kwa Mungu.
- 3 Tena, mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu.
- 4 Ninyi ni watu msio na uaminifu kama wazinzi. Je, hamjui kwamba kuwa rafiki wa ulimwengu ni kuwa adui wa Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa ulimwengu anajifanya adui wa Mungu.
- 5 Msifikiri kwamba Maandiko Matakatifu yamesema maneno ya bure, yanaposema: "Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu ana wivu mkubwa."
- 6 Lakini, neema tunayopewa na Mungu ina nguvu zaidi; kama yasemavyo Maandiko: "Mungu huwapinga wenye majivuno lakini huwapa neema wanyenyekevu."
- 7 Basi, jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Ibilisi naye atawakimbieni.
- 8 Mkaribieni Mungu, naye atakuja karibu nanyi. Osheni mikono yenu enyi wakosefu! Safisheni mioyo yenu enyi wanafiki!
- 9 Oneni huzuni, lieni na kuomboleza; kicheko chenu na kiwe kilio; na furaha yenu iwe huzuni kubwa.
- 10 Nyenyekeeni mbele ya Bwana, naye atawainueni.
- 11 Ndugu, msilaumiane ninyi kwa ninyi. Anayemlaumu ndugu yake na kumhukumu, huyo huilaumu na kuihukumu Sheria. Kama ukiihukumu Sheria, basi, wewe huitii Sheria, bali waihukumu.
- 12 Mungu peke yake ndiye mwenye kuweka Sheria na kuhukumu. Ni yeye peke yake anayeweza kuokoa na kuangamiza. Basi, wewe ni nani hata umhukumu binadamu mwenzako?
- 13 Basi, sasa sikilizeni ninyi mnaosema: "Leo au kesho tutakwenda katika mji fulani na kukaa huko mwaka mzima tukifanya biashara na kupata faida."
- 14 Ninyi hamjui hata maisha yenu yatakavyokuwa kesho! Ninyi ni kama ukungu unaotokea kwa muda mfupi tu na kutoweka tena.
- 15 Mngalipaswa kusema: "Bwana akitujalia tutaishi na tutafanya hiki au kile."
- 16 Lakini sasa mwajivuna na kujigamba; majivuno ya namna hiyo ni mabaya.
- 17 Basi, mtu ambaye hafanyi lile jambo jema analojua kwamba anapaswa kulifanya, anatenda dhambi.