베드로전서 2장 Swahili NT
- 1 Basi, acheni uovu wote; uongo, unafiki, wivu na maneno ya kashfa visiweko tena.
- 2 Kama vile watoto wachanga wanavyotamani maziwa, nanyi pia mnapaswa kuwa na hamu ya maziwa halisi ya kiroho, ili kwa nguvu yake mpate kukua na kukombolewa.
- 3 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mmegundua kwamba Bwana ni mwema."
- 4 Basi, mwendeeni Bwana! Yeye ndiye jiwe hai lililokataliwa na watu; lakini mbele ya Mungu ni jiwe teule, na la thamani kubwa.
- 5 Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya kiroho, ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea dhabihu za kiroho zenye kumpendeza Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.
- 6 Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Tazama! Naweka huko sioni jiwe kuu la msingi, jiwe la thamani kubwa nililoliteua. Mtu atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa."
- 7 Kwenu ninyi mnaoamini, jiwe hilo ni la thamani kubwa; lakini kwa wale wasioamini, "Jiwe walilokataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi."
- 8 Tena Maandiko yasema: "Jiwe hilo ni jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuwaangusha watu." Watu hujikwaa kwa sababu hawauamini ule ujumbe; na ndivyo walivyopangiwa tangu mwanzo.
- 9 Lakini ninyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani akawaingizeni katika mwanga wake mkuu.
- 10 Wakati mmoja ninyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa ninyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmeipokea.
- 11 Wapenzi wangu, nawasihi ninyi kama wageni na wakimbizi hapa duniani! Achaneni na tamaa za mwili ambazo hupingana na roho.
- 12 Mwenendo wenu kati ya watu wasiomjua Mungu unapaswa kuwa mwema kabisa, ili hata watakapowasingizieni kwamba mnatenda mabaya, waweze kutambua matendo yenu mema na hivyo wamtukuze Mungu Siku ya kuja kwake.
- 13 Basi, jiwekeni chini ya mamlaka yote ya kibinadamu, kwa ajili ya Bwana: utii kwa mfalme aliye mtawala mkuu,
- 14 utii kwa wakuu wa mikoa ambao wameteuliwa naye kuwaadhibu wahalifu na kuwasifu watendao mema.
- 15 Maana Mungu anataka mweze kuyakomesha maneno ya kijinga ya watu wasio na akili kwa matendo mema mnayofanya.
- 16 Ishini kama watu huru; lakini msiutumie uhuru wenu kuuficha ubaya, bali ishini kama watumishi wa Mungu.
- 17 Waheshimuni watu wote, wapendeni ndugu zenu waumini, mcheni Mungu, mheshimuni mfalme.
- 18 Enyi watumishi wa nyumbani, watiini wakuu wenu kwa heshima yote, wawe wema na wapole au wenye kuchukiza.
- 19 Maana kama mnavumilia maumivu ya mateso msiyostahili kwa sababu mwajua kwamba Mungu anataka hivyo, basi Mungu atawafadhili.
- 20 Maana, mtapata tuzo gani mkivumilia mapigo mnayostahili kwa sababu ya makosa yenu? Lakini kama mnavumilia mateso hata ingawa mmetenda mema, Mungu atawapeni baraka kwa ajili hiyo.
- 21 Hayo ndiyo mliyoitiwa; maana Kristo mwenyewe aliteseka kwa ajili yenu, akawaachieni mfano, ili muufuate mwenendo wake.
- 22 Yeye hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika mdomoni mwake.
- 23 Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki.
- 24 Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake juu ya msalaba, tupate kufa kuhusu dhambi, na kuishi kwa ajili ya uadilifu. Kwa majeraha yake, ninyi mmeponywa.
- 25 Ninyi mlikuwa kama kondoo waliokuwa wamepotea; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mlinzi wa roho zenu.