베드로후서 1장 Swahili NT
- 1 Mimi Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia ninyi ambao, kwa wema wake Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo, mmejaliwa imani ileile ya thamani kuu tuliyojaliwa sisi.
- 2 Nawatakieni neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.
- 3 Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji, ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe.
- 4 Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na mpate kuishiriki hali yake ya kimungu.
- 5 Kwa sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza fadhila katika imani yenu: ongezeni elimu katika fadhila yenu,
- 6 kuwa na kiasi katika elimu yenu, uvumilivu katika kuwa na kiasi, uchaji wa Mungu katika uvumilivu wenu,
- 7 udugu katika uchaji wenu, na mapendo katika udugu wenu.
- 8 Mkiwa na sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
- 9 Lakini mtu asiye na sifa hizo ni kipofu, hawezi kuona na amesahau kwamba alikwisha takaswa dhambi zake za zamani.
- 10 Kwa hiyo basi, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo hamtaanguka kamwe.
- 11 Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika Utawala wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
- 12 Kwa hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu, na mko imara katika ukweli mlioupokea.
- 13 Nadhani ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na kuwakumbusheni juu ya mambo haya.
- 14 Najua kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia waziwazi.
- 15 Basi, nitajitahidi kuwapatieni njia ya kuyakumbuka mambo haya kila wakati, baada ya kufariki kwangu.
- 16 Wakati tulipowafundisheni juu ya ukuu wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, hatukutegemea hadithi tupu zisizo na msingi. Sisi tuliuona utukufu wake kwa macho yetu wenyewe.
- 17 Sisi tulikuwapo wakati alipopewa heshima na kutukuzwa na Mungu Baba, wakati sauti ilipomjia kutoka kwake yeye aliye Utukufu Mkuu, ikisema: "Huyu ni Mwanangu mpenzi, nimependezwa naye."
- 18 Tena, sisi wenyewe tulisikia sauti hiyo kutoka mbinguni wakati tulipokuwa pamoja naye juu ya ule mlima mtakatifu.
- 19 Tena, ujumbe wa manabii watuthibitishia jambo hilo; nanyi mwafanya vema kama mkiuzingatia, maana ni kama taa inayoangaza mahali penye giza mpaka Siku ile itakapopambazuka na mwanga wa nyota ya asubuhi utakapong'ara mioyoni mwenu.
- 20 Zaidi ya hayo, lakini, kumbukeni kwamba hakuna mtu yeyote awezaye kufafanua mwenyewe unabii ulio katika Maandiko Matakatifu.
- 21 Maana hakuna ujumbe wa kinabii unaotokana na matakwa ya binadamu, bali watu walinena ujumbe wa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.