요한일서 1장 Swahili NT
- 1 Habari hii ya yahusu Neno la uzima lililokuwako tangu mwanzo. Sisi tumepata kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa mikono yetu wenyewe.
- 2 Uzima huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uzima huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu.
- 3 Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni ninyi pia ili nanyi mpate kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo.
- 4 Tunawaandikia ninyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike.
- 5 Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake.
- 6 Tukisema kwamba tuna umoja naye, na papo hapo twaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo kwa maneno na matendo.
- 7 Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote.
- 8 Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe na ukweli haumo ndani yetu.
- 9 Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa na uovu wote.
- 10 Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.