요한일서 3장 Swahili NT
- 1 Oneni basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu.
- 2 Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo.
- 3 Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa.
- 4 Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa sheria.
- 5 Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na kwamba kwake hamna dhambi yoyote.
- 6 Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi dhambi; lakini kila mtu atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona, wala kumjua Kristo.
- 7 Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote. Mtu atendaye matendo maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu kabisa.
- 8 Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi ametenda dhambi tangu mwanzo. Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu kazi ya Ibilisi.
- 9 Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo hali ya kimungu ndani yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa Mungu.
- 10 Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi.
- 11 Na, ujumbe mliousikia tangu mwanzo ndio huu: Tunapaswa kupendana!
- 12 Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu, alimuua ndugu yake. Na, kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu, lakini yale ya ndugu yake yalikuwa mema!
- 13 Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia ninyi.
- 14 Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uzima kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo.
- 15 Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua kwamba muuaji yeyote yule hana uzima wa milele ndani yake.
- 16 Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu.
- 17 Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu?
- 18 Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa vitendo.
- 19 Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni watu wa ukweli; na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu.
- 20 Kwa maana, hata kama dhamiri yetu yatuhukumu, twajua kwamba Mungu ni mkuu zaidi kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu.
- 21 Wapenzi wangu, kama dhamiri yetu haina lawama juu yetu, basi, twaweza kuwa na uthabiti mbele ya Mungu,
- 22 na twaweza kupokea kwake chochote tunachoomba, maana tunazitii amri zake na kufanya yale yanayompendeza.
- 23 Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Kristo, na kupendana kama alivyotuamuru.
- 24 Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia, sisi twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi.