요한계시록 10장 Swahili NT
- 1 Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu, na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama moto.
- 2 Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa. Aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari, na wa kushoto juu ya nchi kavu,
- 3 na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba. Alipopaaza sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo.
- 4 Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika. Lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni: "Maneno ya ngurumo hizo saba ni siri; usiyaandike!"
- 5 Kisha yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni,
- 6 akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote vilivyomo. Akasema, "Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha!
- 7 Lakini wakati ule malaika wa saba atakapotoa sauti yake, wakati atakapopiga tarumbeta yake, Mungu atakamilisha mpango wake wa siri kama alivyowatangazia watumishi wake manabii."
- 8 Kisha ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni pale awali ikasema nami tena: "Nenda ukakichukue kile kitabu kilichofunguliwa, kilicho mkononi mwa malaika asimamaye juu ya bahari na juu ya nchi kavu."
- 9 Basi, nikamwendea huyo malaika, nikamwambia anipe hicho kitabu kidogo. Naye akaniambia, "Kichukue, ukile; kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali, lakini tumboni kitakuwa kichungu!"
- 10 Basi, nikakichukua kitabu hicho kidogo kutoka mkononi mwa huyo malaika, nikakila; nacho kilikuwa kitamu kinywani mwangu kama asali, lakini nilipokimeza kikawa kichungu tumboni mwangu.
- 11 Kisha nikaambiwa, "Inakubidi tena kutangaza ujumbe wa Mungu kuhusu watu wengi, mataifa, watu wa lugha nyingi na wafalme!"