마태복음 14장 Swahili NT
- 1 Wakati huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu.
- 2 Basi, akawaambia watumishi wake, "Mtu huyu ni Yohane mbatizaji, amefufuka kutoka wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake."
- 3 Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Sababu hasa ni
- 4 kwamba alikuwa amemwambia Herode, "Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!"
- 5 Herode alitaka kumwua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii.
- 6 Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa,
- 7 hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba.
- 8 Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, "Nipe papahapa katika sinia kichwa cha Yohane mbatizaji."
- 9 Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe.
- 10 Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane.
- 11 Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake.
- 12 Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu.
- 13 Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini.
- 14 Basi, aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya wagonjwa wao.
- 15 Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, "Mahali hapa ni nyikani, na saa zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula."
- 16 Yesu akawaambia, "Si lazima waende, wapeni ninyi chakula."
- 17 Lakini wao wakamwambia, "Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili."
- 18 Yesu akawaambia, "Nileteeni hapa."
- 19 Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu. Halafu akaimega hiyo mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu.
- 20 Watu wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu kumi na viwili.
- 21 Jumla ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.
- 22 Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ng'ambo ya ziwa wakati yeye anawaaga watu.
- 23 Baada ya kuwaaga, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake,
- 24 na wakati huo ile mashua ilikwishafika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikuwa inakwenda mrama kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga.
- 25 Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji.
- 26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliingiwa na hofu, wakasema, "Ni mzimu!" Wakapiga kelele kwa hofu.
- 27 Mara, Yesu akasema nao, "Tulieni, ni mimi. Msiogope!"
- 28 Petro akamwambia, "Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako."
- 29 Yesu akasema, "Haya, njoo." Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu.
- 30 Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, "Bwana, niokoe!"
- 31 Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, "Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?"
- 32 Basi, wakapanda mashuani, na upepo ukatulia.
- 33 Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, "Hakika wewe ni Mwana wa Mungu."
- 34 Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti.
- 35 Watu wa huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea Yesu wagonjwa wote,
- 36 wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake; wote waliomgusa walipona.