마태복음 27장 Swahili NT
- 1 Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumwua.
- 2 Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato, mkuu wa mkoa.
- 3 Hapo, Yuda ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu zile sarafu thelathini za fedha.
- 4 Akawaambia, "Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia auawe." Lakini wao wakasema, "Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri lako."
- 5 Naye akazitupa zile fedha Hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga.
- 6 Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, "Haifai kuziweka katika hazina ya Hekalu kwa maana ni fedha za damu."
- 7 Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.
- 8 Ndiyo maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu.
- 9 Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: "Walizichukua sarafu thelathini za fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walipanga bei,
- 10 wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza."
- 11 Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, "Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?" Yesu akamwambia, "Wewe umesema."
- 12 Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno.
- 13 Hivyo Pilato akamwuliza, "Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?"
- 14 Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana.
- 15 Ilikuwa kawaida wakati wa Sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka.
- 16 Wakati huo kulikuwa na mfungwa mmoja, jina lake Baraba.
- 17 Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, "Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba ama Yesu aitwae Kristo?"
- 18 Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu.
- 19 Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: "Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake."
- 20 Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe.
- 21 Mkuu wa mkoa akawauliza, "Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?" Wakamjibu, "Baraba!"
- 22 Pilato akawauliza, "Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?" Wote wakasema, "Asulubiwe!"
- 23 Pilato akauliza, "Kwa nini? Amefanya kosa gani?" Wao wakazidi kupaaza sauti: "Asulubiwe!"
- 24 Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, "Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe."
- 25 Watu wote wakasema, "Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!"
- 26 Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, lakini akamtoa Yesu asulubiwe.
- 27 Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima.
- 28 Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu.
- 29 Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, "Shikamoo mfalme wa Wayahudi!"
- 30 Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani.
- 31 Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.
- 32 Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu.
- 33 Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, "Mahali pa Fuvu la kichwa,"
- 34 wakampa mchanganyiko wa divai na nyongo. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa.
- 35 Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.
- 36 Wakaketi, wakawa wanamchunga.
- 37 Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lilioandikwa, "Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi."
- 38 Wanyang'anyi wawili walisulubishwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia.
- 39 Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema,
- 40 "Wewe! Si ulijidai kulivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi shuka msalabani!"
- 41 Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na walimu wa Sheria na wazee walimdhihaki wakisema,
- 42 "Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Eti yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini.
- 43 Alimtumainia Mungu na kusema eti yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka."
- 44 Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana.
- 45 Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, nchi yote ikawa katika giza.
- 46 Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eli, Eli, lema sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?"
- 47 Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, "Anamwita Eliya."
- 48 Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe.
- 49 Wengine wakasema, "Acha tuone kama Eliya anakuja kumwokoa."
- 50 Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho.
- 51 Hapo pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;
- 52 makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa;
- 53 nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika Mji Mtakatifu, wakaonekana na watu wengi.
- 54 Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, "Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu."
- 55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia.
- 56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo.
- 57 Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa Armathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu.
- 58 Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi, Pilato akaamuru apewe.
- 59 Yosefu akauchukua ule mwili akauzungushia sanda safi ya kitani,
- 60 akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.
- 61 Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi kulielekea kaburi.
- 62 Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato,
- 63 Wakasema, "Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, Baada ya siku tatu nitafufuka.
- 64 Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa awali."
- 65 Pilato akawaambia, "Haya, mnao walinzi; nendeni mkalinde kadiri mjuavyo."
- 66 Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi.