마태복음 28장 Swahili NT
- 1 Baada ya Sabato, karibu na mapambazuko ya siku ile ya Jumapili, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kutazama lile kaburi.
- 2 Ghafla kutatokea tetemeko kubwa la nchi; malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akalivingirisha lile jiwe, akalikalia.
- 3 Alionekana kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji.
- 4 Walinzi wa lile kaburi wakatetemeka kwa hofu kubwa, hata wakawa kama wamekufa.
- 5 Lakini yule malaika akawaambia wale wanawake, "Ninyi msiogope! Najua kwamba mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa.
- 6 Hayupo hapa maana amefufuka kama alivyosema. Njoni mkaone mahali alipokuwa amelala.
- 7 Basi, nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba amefufuka kutoka wafu, na sasa anawatangulieni kule Galilaya; huko mtamwona. Haya, mimi nimekwisha waambieni."
- 8 Wakiwa wenye hofu na furaha kubwa, hao wanawake walitoka upesi kaburini, wakakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi wake.
- 9 Mara, Yesu akakutana nao, akawasalimu: "Salamu." Hao wanawake wakamwendea, wakapiga magoti mbele yake, wakashika miguu yake.
- 10 Kisha Yesu akawaambia, "Msiogope! Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, na huko wataniona."
- 11 Wale wanawake walipokuwa wanakwenda zao, baadhi ya walinzi wa lile kaburi walikwenda mjini kutoa taarifa kwa makuhani wakuu juu ya mambo yote yaliyotukia.
- 12 Basi, wakakutana pamoja na wazee, na baada ya kushauriana, wakawapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha
- 13 wakisema, "Ninyi mtasema hivi: Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tukiwa tumelala.
- 14 Na kama mkuu wa mkoa akijua jambo hili, sisi tutasema naye na kuhakikisha kuwa ninyi hamtapata matatizo."
- 15 Wale walinzi wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Habari hiyo imeenea kati ya Wayahudi mpaka leo.
- 16 Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya kwenye ule mlima aliowaagiza Yesu.
- 17 Walipomwona, wakamwabudu, ingawa wengine walikuwa na mashaka.
- 18 Yesu akaja karibu, akawaambia, "Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.
- 19 Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu; mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.
- 20 Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati."