마태복음 3장 Swahili NT
- 1 Siku hizo Yohane Mbatizaji alitokea, akaanza kuhubiri katika jangwa la Yudea:
- 2 "Tubuni, maana Ufalme wa mbinguni umekaribia."
- 3 Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu yake aliposema: "Sauti ya mtu imesikika jangwani: Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni vijia vyake."
- 4 Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.
- 5 Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka mkoa wote wa Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea,
- 6 wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.
- 7 Lakini alipowaona Mafarisayo wengi na Masadukayo wanamjia ili awabatize, aliwaambia, "Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea kwamba mnaweza kuiepuka ghadhabu inayokuja?
- 8 Onyesheni basi kwa matendo, kwamba mmetubu kweli.
- 9 Msidhani kwamba mtaweza kujitetea kwa kusema, Baba yetu ni Abrahamu! Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu.
- 10 Basi, shoka liko tayari kuikata mizizi ya miti; hivyo, kila mti usiozaa matunda mazuri, utakatwa na kutupwa motoni.
- 11 Mimi ninawabatizeni kwa maji kuonyesha kwamba mmetubu. Lakini yule anayekuja baada yangu ana uwezo kuliko mimi. Mimi sistahili hata kubeba viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.
- 12 Yeye anashika mkononi chombo cha kupuria nafaka, ili aipure nafaka yake; akusanye ngano ghalani, na makapi ayachome kwa moto usiozimika."
- 13 Wakati huo Yesu alitoka Galilaya akafika katika mto Yordani, akamwendea Yohane ili abatizwe naye.
- 14 Lakini Yohane alijaribu kumzuia akisema, "Je, wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe."
- 15 Lakini Yesu akamjibu, "Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana kwa namna hii inafaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka." Hapo Yohane akakubali.
- 16 Mara tu Yesu alipokwisha batizwa, alitoka majini; na ghafla mbingu zikafunguka, akaona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa na kutua juu yake.
- 17 Sauti kutoka mbinguni ikasema, "Huyu ndiye Mwanangu mpendwa, nimependezwa naye."