누가복음 17장 Swahili NT
- 1 Kisha, Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Haiwezekani kabisa kusitokee vikwazo vinavyosababisha dhambi; lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha.
- 2 Ingekuwa afadhali kwake kufungiwa shingoni jiwe kubwa la kusagia na kutoswa baharini, kuliko kumkwaza mmoja wa wadogo hawa.
- 3 Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, mwonye; akitubu, msamehe.
- 4 Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema Nimetubu, lazima umsamehe."
- 5 Mitume wakamwambia Bwana, "Utuongezee imani."
- 6 Naye Bwana akajibu, "Kama imani yenu ingekuwa ndogo hata kama chembe ndogo ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu: Ng'oka ukajipandikize baharini, nao ungewatii.
- 7 "Tuseme mmoja wenu ana mtumishi ambaye analima shambani au anachunga kondoo. Je, anaporudi kutoka shambani, atamwambia: Haraka, njoo ule chakula?
- 8 La! Atamwambia: Nitayarishie chakula, ujifunge tayari kunitumikia mpaka nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo nawe ule na unywe.
- 9 Je utamshukuru huyo mtumishi kwa sababu ametimiza aliyoamriwa?
- 10 Hali kadhalika na ninyi mkisha fanya yote mliyoamriwa, semeni: Sisi ni watumishi tusio na faida, tumetimiza tu yale tuliyotakiwa kufanya."
- 11 Yesu akiwa safarini kwenda Yerusalemu alipitia mipakani mwa Samaria na Galilaya.
- 12 Alipokuwa anaingia katika kijiji kimoja, watu kumi wenye ukoma walikutana naye, wakasimama kwa mbali.
- 13 Wakapaza sauti wakisema, "Yesu Mwalimu, tuonee huruma!"
- 14 Alipowaona akawaambia, "Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani." Basi, ikawa walipokuwa wanakwenda, wakatakasika.
- 15 Mmoja wao alipoona kwamba ameponywa alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa.
- 16 Akajitupa chini mbele ya miguu ya Yesu huku akimshukuru. Huyo alikuwa Msamaria.
- 17 Hapo Yesu akasema, "Je, si watu kumi walitakaswa? Wale tisa wako wapi?
- 18 Hakupatikana mwingine aliyerudi kumtukuza Mungu ila tu huyu mgeni?"
- 19 Halafu akamwambia huyo mtu, "Simama, uende zako; imani yako imekuponya."
- 20 Wakati mmoja, Mafarisayo walimwuliza Yesu, "Ufalme wa Mungu utakuja lini?" Naye akawajibu, "Ufalme wa Mungu hauji kwa namna itakayoweza kuonekana.
- 21 Wala hakuna atakayeweza kusema, Uko hapa, au Uko pale. Kwa kweli Ufalme wa Mungu uko kati yenu."
- 22 Halafu akawaambia wanafunzi wake, "Siku zinakuja ambapo mtatamani kuona mojawapo ya siku za Mwana wa Mtu, lakini hamtaiona.
- 23 Na watu watawaambieni: Tazameni yuko hapa; ninyi msitoke wala msiwafuate.
- 24 Kwa maana kama vile umeme unavyotokea ghafla na kuangaza anga upande mmoja hadi mwingine, ndivyo Mwana wa Mtu atakavyokuwa siku yake.
- 25 Lakini kabla ya hayo, itambidi ateseke sana na kukataliwa na kizazi hiki.
- 26 Kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Mtu.
- 27 Watu waliendelea kula na kunywa, kuoa na kuolewa mpaka wakati ule Noa alipoingia katika safina. Gharika ikatokea na kuwaangamiza wote.
- 28 Itakuwa kama ilivyotokea wakati wa Loti. Watu waliendelea kula na kunywa, kununua na kuuza, kupanda mbegu na kujenga.
- 29 Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, moto na kiberiti vikanyesha kama mvua kutoka mbinguni na kuwaangamiza wote.
- 30 Ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Mtu atakapofunuliwa.
- 31 "Siku hiyo, yeyote atakayekuwa juu ya paa asishuke nyumbani kuchukua mali yake. Kadhalika, naye atakayekuwa shambani asirudi nyuma.
- 32 Kumbukeni yaliyompata mke wa Loti.
- 33 Yeyote anayetaka kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na yeyote anayeipoteza, ataiokoa.
- 34 Nawaambieni, siku ile usiku watu wawili watakuwa wanalala pamoja, mmoja atachukuliwa na yule mwingine ataachwa.
- 35 Wanawake wawili watakuwa wakisaga nafaka pamoja; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa."
- 36 Watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
- 37 Hapo wakamwuliza, "Ni wapi Bwana?" Naye akawaambia, "Ulipo mzoga, ndipo tai watakapokusanyikia."