누가복음 18장 Swahili NT
- 1 Basi, Yesu aliwasimulia mfano kuonyesha kwamba ni lazima kusali daima bila kukata tamaa.
- 2 Alisema: "Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu ambaye hakuwa anamcha Mungu wala kumjali binadamu.
- 3 Katika mji huohuo, kulikuwa pia na mama mmoja mjane, ambaye alimwendea huyo hakimu mara nyingi akimwomba amtetee apate haki yake kutoka kwa adui yake.
- 4 Kwa muda mrefu huyo hakimu hakupenda kumtetea huyo mjane; lakini, mwishowe akajisemea: Ingawa mimi simchi Mungu wala simjali binadamu,
- 5 lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua, nitamtetea; la sivyo ataendelea kufika hapa, na mwisho atanichosha kabisa!"
- 6 Basi, Bwana akaendelea kusema, "Sikieni jinsi alivyosema huyo hakimu mbaya.
- 7 Je, ndio kusema Mungu hatawatetea wale aliowachagua, ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasikiliza?
- 8 Nawaambieni atawatetea upesi. Hata hivyo, je, kutakuwako na imani duniani wakati Mwana wa Mtu atakapokuja?"
- 9 Halafu Yesu aliwaambia pia mfano wa wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau wengine.
- 10 "Watu wawili walipanda kwenda Hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo, na mwingine mtoza ushuru.
- 11 Huyo Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtoza ushuru.
- 12 Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.
- 13 Lakini yule mtoza ushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi.
- 14 Nawaambieni, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa."
- 15 Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali.
- 16 Lakini Yesu akawaita kwake akisema: "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa.
- 17 Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hataingia katika Ufalme huo."
- 18 Kiongozi mmoja, Myahudi, alimwuliza Yesu, "Mwalimu mwema, nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?"
- 19 Yesu akamwambia, "Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.
- 20 Unazijua amri: Usizini; usiue; usiibe; usitoe ushahidi wa uongo; waheshimu baba yako na mama yako."
- 21 Yeye akasema, "Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu."
- 22 Yesu aliposikia hayo akamwambia, "Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: uza kila ulicho nacho, wagawie maskini, na hivyo utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu njoo unifuate."
- 23 Lakini huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana.
- 24 Yesu alipoona akihuzunika hivyo, akasema, "Jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!
- 25 Naam, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu."
- 26 Wale watu waliposikia hayo, wakasema, "Nani basi, atakayeokolewa?"
- 27 Yesu akajibu, "Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu."
- 28 Naye Petro akamwuliza, "Na sisi je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!"
- 29 Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au kaka au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu,
- 30 atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na kupokea uzima wa milele wakati ujao."
- 31 Yesu aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, "Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu kitakamilishwa.
- 32 Kwa maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate.
- 33 Watampiga mijeledi, watamuua; lakini siku ya tatu atafufuka."
- 34 Lakini wao hawakuelewa hata kidogo jambo hilo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno hayo, na hawakutambua yaliyosemwa.
- 35 Wakati Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu ameketi njiani akiomba.
- 36 Aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza, "Kuna nini?"
- 37 Wakamwambia, "Yesu wa Nazareti anapita."
- 38 Naye akapaza sauti akisema, "Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!"
- 39 Wale watu waliotangulia wakamkemea wakimwambia anyamaze; lakini yeye akazidi kupaza sauti: "Mwana wa Daudi, nihurumie;"
- 40 Yesu alisimama, akaamuru wamlete mbele yake. Yule kipofu alipofika karibu, Yesu akamwuliza,
- 41 "Unataka nikufanyie nini?" Naye akamjibu, "Bwana, naomba nipate kuona tena."
- 42 Yesu akamwambia, "Ona! Imani yako imekuponya."
- 43 Na mara yule aliyekuwa kipofu akapata kuona, akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu.