누가복음 19장 Swahili NT
- 1 Yesu aliingia mjini Yeriko, akawa anapita katika njia za mji huo.
- 2 Kulikuwa na mtu mmoja mjini, jina lake Zakayo ambaye alikuwa mkuu wa watoza ushuru tena mtu tajiri.
- 3 Alitaka kuona Yesu alikuwa nani, lakini kwa sababu ya umati wa watu, na kwa vile alikuwa mfupi, hakufaulu.
- 4 Hivyo, alitangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu ili aweze kumwona Yesu, kwa maana alikuwa apitie hapo.
- 5 Basi, Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu akamwambia, "Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako."
- 6 Zakayo akashuka haraka, akamkaribisha kwa furaha.
- 7 Watu wote walipoona hayo, wakaanza kunung'unika wakisema, "Amekwenda kukaa kwa mtu mwenye dhambi."
- 8 Lakini Zakayo akasimama akamwambia Yesu, "Sikiliza Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyang'anya mtu yeyote kitu, nitamrudishia mara nne."
- 9 Yesu akamwambia, "Leo wokovu umefika katika nyumba hii, kwa vile huyu pia ni wa ukoo wa Abrahamu.
- 10 Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa waliopotea."
- 11 Wakati watu walipokuwa bado wanasikiliza hayo, Yesu akawaambia mfano. (Hapo alikuwa anakaribia Yerusalemu, na watu wale walidhani kwamba muda si muda, Ufalme wa Mungu ungefika.)
- 12 Hivyo akawaambia, "Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa kifalme aliyefanya safari kwenda nchi ya mbali ili apokee madaraka ya ufalme, halafu arudi.
- 13 Basi, kabla ya kuondoka aliwaita watumishi wake kumi, akawapa kiasi cha fedha kila mmoja na kumwambia: Fanyeni nazo biashara mpaka nitakaporudi.
- 14 Lakini wananchi wenzake walimchukia na hivyo wakatuma wajumbe waende wakaseme: Hatumtaki huyu atutawale.
- 15 "Huyo mtu mashuhuri alirudi nyumbani baada ya kufanywa mfalme, na mara akaamuru wale watumishi aliowapa zile fedha waitwe ili aweze kujua kila mmoja amepata faida gani.
- 16 Mtumishi wa kwanza akatokea, akasema: Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara kumi ya zile fedha ulizonipa.
- 17 Naye akamwambia: Vema; wewe ni mtumishi mwema. Kwa kuwa umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi!
- 18 Mtumishi wa pili akaja, akasema: Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara tano ya zile fedha ulizonipa.
- 19 Naye akamwambia pia: Nawe utakuwa na madaraka juu ya miji mitano.
- 20 "Mtumishi mwingine akaja, akasema: Chukua fedha yako; niliificha salama katika kitambaa,
- 21 kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na huchuma ambacho hukupanda.
- 22 Naye akamwambia: Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu na kuchuma nisichopanda.
- 23 Kwa nini basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?
- 24 Hapo akawaambia wale waliokuwa pale: Mnyang'anyeni hizo fedha, mkampe yule aliyepata faida mara kumi.
- 25 Nao wakamwambia: Lakini Mheshimiwa, huyo ana faida ya kiasi hicho mara kumi!
- 26 Naye akawajibu: Kila aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.
- 27 Na sasa, kuhusu hao maadui wangu ambao hawapendi niwe mfalme wao, waleteni hapa, mkawaue papa hapa mbele yangu."
- 28 Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu.
- 29 Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,
- 30 akawaambia: "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana punda amefungwa ambaye hajatumiwa na mtu. Mfungeni, mkamlete hapa.
- 31 Kama mtu akiwauliza, kwa nini mnamfungua, mwambieni, Bwana ana haja naye."
- 32 Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia.
- 33 Walipokuwa wanamfungua yule mwana punda, wenyewe wakawauliza, "Kwa nini mnamfungua mwana punda huyu?"
- 34 Nao wakawajibu, "Bwana anamhitaji."
- 35 Basi, wakampelekea Yesu yule mwana punda. Kisha wakatandika mavazi yao juu yake wakampandisha Yesu.
- 36 Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi yao barabarani.
- 37 Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake, wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa, kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona;
- 38 wakawa wanasema: "Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!"
- 39 Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi la watu, wakamwambia Yesu, "Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!"
- 40 Yesu akawajibu, "Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti."
- 41 Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia
- 42 akisema: "Laiti ungelijua leo hii yale yaletayo amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako.
- 43 Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma, watakuzingira na kukusonga pande zote.
- 44 Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu jingine, kwa sababu hukuutambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa."
- 45 Kisha, Yesu aliingia Hekaluni, akaanza kuwafukuzia nje wafanyabiashara
- 46 akisema, "Imeandikwa: Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi."
- 47 Yesu akawa anafundisha kila siku Hekaluni. Makuhani wakuu, walimu wa Sheria na viongozi wa watu walitaka kumwangamiza,
- 48 lakini hawakuwa na la kufanya, maana watu wote walikuwa wakimsikiliza kwa makini kabisa.