누가복음 1장 Swahili NT
- 1 Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu.
- 2 Waliandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo.
- 3 Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango,
- 4 ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa.
- 5 Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni.
- 6 Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama.
- 7 Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.
- 8 Siku moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu,
- 9 Zakariya alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani.
- 10 Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani.
- 11 Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani.
- 12 Zakariya alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.
- 13 Lakini malaika akamwambia, "Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane.
- 14 Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.
- 15 Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake.
- 16 Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao.
- 17 Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake."
- 18 Zakariya akamwambia huyo malaika, "Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu."
- 19 Malaika akamjibu, "Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa niseme nawe, nikuletee hii habari njema.
- 20 Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia."
- 21 Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia kwake Hekaluni.
- 22 Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu.
- 23 Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani.
- 24 Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema:
- 25 "Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu."
- 26 Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya,
- 27 kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi.
- 28 Malaika akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe."
- 29 Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini?
- 30 Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema.
- 31 Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu.
- 32 Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake.
- 33 Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho."
- 34 Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?"
- 35 Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu.
- 36 Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa.
- 37 Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu."
- 38 Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake.
- 39 Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda.
- 40 Huko, aliingia katika nyumba ya Zakariya, akamsalimu Elisabeti.
- 41 Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifiu,
- 42 akasema kwa sauti kubwa, "Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa.
- 43 Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?
- 44 Nakwambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha.
- 45 Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokwambia."
- 46 Naye Maria akasema,
- 47 "Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
- 48 Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
- 49 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu.
- 50 Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.
- 51 Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
- 52 amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu.
- 53 Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
- 54 Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake.
- 55 Kama alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele."
- 56 Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake.
- 57 Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume.
- 58 Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye.
- 59 Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakariya.
- 60 Lakini mama yake akasema, "La, sivyo, bali ataitwa Yohane."
- 61 Wakamwambia, "Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?"
- 62 Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani.
- 63 Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: "Yohane ndilo jina lake." Wote wakastaajabu.
- 64 Papo hapo midomo na ulimi wake Zakariya vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu.
- 65 Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea.
- 66 Wote waliosikia mambo hayo waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: "Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?" Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
- 67 Zakariya, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka ujumbe wa Mungu:
- 68 "Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amekuja kuwasaidia na kuwakomboa watu wake.
- 69 Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake.
- 70 Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu,
- 71 kwamba atatuokoa mikononi mwa adui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia.
- 72 Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu.
- 73 Kiapo alichomwapia Abrahamu baba yetu, ni kwamba atatujalia sisi
- 74 tukombolewe kutoka adui zetu, tupate kumtumikia bila hofu,
- 75 kwa unyofu na uadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu.
- 76 Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake;
- 77 kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao.
- 78 Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atasababisha pambazuko angavu la ukombozi litujie kutoka juu,
- 79 na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani."
- 80 Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionyesha rasmi kwa watu wa Israeli.